Netumbo Nandi-Ndaitwah kwa jina maarufu NNN, ameandikisha historia baada ya kuchaguliwa kama rais wa kwanza mwanamke nchini Namibia.
Akiwa na umri wa miaka 72 alishinda uchaguzi kwa 57% ya kura huku mpinzani wake wa karibu Panduleni Itula akipata 26% ya kura, kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo.
Ni kisa katika mfululizo wa matukio katika maisha yake- Nandi-Ndaitwah akipigana na utawala uliokuwa, na kutoroka kisha kujiwezesha na kujijenga kama mwanamke mashuhuri nchini Namibia.
Hata hivyo Itula amepinga vikali ushindi wake. Alisema uchaguzi ulikumbwa na dosari nyingi na kusababisha upigaji kura kuongezewa muda wa siku tatu katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika taifa hilo.
Chama chake cha kisiasa alichogombea nacho cha Independent Patriots for Change (IPC) kimedokeza kuwasalisha malalamiko yao dhidi ya uchaguzi huo katika mahakama .
Nandi-Ndaitwah amekuwa mwanachama mwaminifu chama tawala cha SWAPO tangu akiwa msichana na kuapa kuleta mabadiliko ya kiuchumi Namibia.
Nandi-Ndaitwa alizaliwa 1952 ,kaskazini mwa kijiji cha Onamutai.
Ni mtoto wa tisa miongoni mwa watoto 13 na babake mzazi alikuwa kiongozi wa kidini wa kanisa la Anglikana.
Wakati huo, Namibia ikijulikana kama Kusini magharibi mwa Afrika na watu wakiwa chini ya utawala wa Afrika kusini.
Nandi-Ndaitwah alijiunga na chama cha Swapo, wakati huo vuguvugu la ukombozi lililopinga utawala wa wazungu wachache wa Afrika Kusini, alipokuwa na umri wa miaka 14 pekee.
Mwanaharakati mwenye ukakamavu, Nandi-Ndaitwah alikua kiongozi wa kitengo cha vijana katika chama cha Swapo.
Jukumu hilo lilimtengenezea maisha ya kisiasa yenye mafanikio, lakini wakati huo Nandi-Ndaitwah alikuwa na nia ya kuikomboa Afrika Kusini Magharibi.
"Siasa ziliingia kwa sababu ya mazingira. Ningekuwa labda mwanasayansi, "alisema katika mahojiano mwaka huu.
Akiwa bado ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ,Nandi-Ndaitwah alikamatwa na kuzuiliwa wakati msako wa wanaharakati wa Swapo .
Kufuatia haya, aliamua kuondoka nchini Namibia na kujumuika na wanaharakati wenzake wa SWAPO waliokuwa uhamishoni.
Aliendelea kupanga vuguvugu akiwa Zambia na Tanzania ,kabla ya kuelekea Uingereza kusoma shahada ya mahusiano ya kimataifa.
Mnamo mwaka wa 1988- miaka 14 tangu Nandi- Ndaitwah aondoke nchini kwao-Afrika kusini ilikubali kuachia Namibia iwe huru.
Nandi-Ndaitwah alirejea nyumbani na kujiunga na serikali iliyochukua madaraka baada ya uhuru.
Kwa miaka amekuwa akishikilia wadhifa mbalimbali ikiwemo majukumu ya waziri katika wizara kama vile masuala ya kigeni,utalii ,ustawi wa watoto na mawasiliano.
Nandi-Ndaitwah pia alifahamika kama mtetezi wa haki za wanawake nchini humo.
Katika masuala anayojivunia ni kuwa alishinikiza sheria ya kukabiliana na unyanyanyasaji dhidi ya jinsia ya kike kupitia bunge la taifa.
Kulingana na vyombo vya habari Namibia, Nandi-Ndaitwah aliwasuta wenzake wa kiume waliokuwa wakipuuzilia mbali sheria hiyo akiwakumbusha kuwa Katiba ya chama cha Swampo haikubali taasubi za kiume.
Aliendelea kupaa katika uongozi katika nchi iliyojaa ubepari na siasa zilizojaa wanaume,na mwezi Februari mwaka huu akawa makamu wa rais.
Alimrithi Nangolo Mbumba ambaye alichukua nafasi ya urais baada ya rais aliyekuwepo Hage Geingob kufariki.
Katika maisha yake ya kibinafsi,Nandi-Ndaitwah ameolewa na Epaphras Denga Ndaitwah,aliyekuwa mkuu wa idara ya ulinzi nchini Namibia.
Wakibarikiwa na wavulana watatu.
Katika tajriba yake akiwa kazini ,Nandi- Ndaitwah amekuwa ni mchapakazi ,na mtendaji katika uongozi wake.
Wakati mmoja amewahi kunadi :''Mimi ni mtekelzaji,sio mpiga soga