Wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini inasema balozi wa Marekani "ameomba radhi" kwa kudai kuwa nchi hiyo iliiuzia Urusi silaha.
Siku ya Alhamisi Reuben Brigety alidai meli ya Urusi ilikuwa imesheheni risasi na silaha huko mjini Cape Town Disemba mwaka jana.
Afrika Kusini inasema haina rekodi ya mauzo ya silaha na Rais Cyril Ramaphosa ameagiza uchunguzi ufanyike.
Siku ya Ijumaa msemaji wa masuala ya usalama wa taifa wa Ikulu ya White House hakusema lolote kuhusu maelezo ya madai hayo.
Lakini John Kirby alisema ni "suala zito" na Marekani imekuwa ikizitaka nchi mara kwa mara kutounga mkono vita vya Urusi nchini Ukraine.
Akiandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya kukutana na wizara ya mambo ya nje, Bw Brigety alisema "anashukuru kwa fursa ya... kurekebisha maoni yoyote potofu yaliyotokana na matamshi yangu hadharani".
Alisema katika mazungumzo hayo "uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya nchi zetu mbili na ajenda muhimu ambayo marais wetu wametupa".
Wakati huo huo waziri wa baraza la mawaziri la Afrika Kusini alikosoa "diplomasia ya aina hiyo, akisema Afrika Kusini haiwezi "kuonewa na Marekani".