AMUUA MKE WAKE BAADA YA KUKATAA KUMLIPIA BODA BODA

Admin
By -
0
MWANAMKE mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Minza Paul (25) amefariki dunia mkoani Mbeya kwa kucharazwa bakora na mumewe hadi mauti yalipomfika.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga aliwaambia waandishi wa habari katika taarifa yake ya jana kuwa mbali na Minza, mwanaume mmoja pia alifariki dunia katika tukio tofauti.

Katika taarifa yake hiyo, Kamanda Mpinga alisema kuwa tukio la kwanza linalohusiana na kuuawa kwa Minza, lilitokea juzi katika kijiji cha Ipwizi, Kata ya Mjele wilayani Mbeya ambapo inadaiwa majira ya saa 4:06 usiku mumewe aliyemtaja kwa jina la Shilondi Mwakwenge, alianza kumshambulia kwa kumpiga na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake.

Alisema kuwa chanzo cha ugomvi huo kilikuwa ni Shilondi kurejea nyumbani usiku akiwa amelewa huku akiwa amekodi bodaboda, na alipofika nyumbani alimwamuru mkewe huyo kumlipa dereva wa pikipiki.

Kwa mujibu wa Kamanda Mpinga, marehemu Minza alidai hana fedha za kumlipa dereva wa bodaboda na ndipo ugomvi ulipoibuka baina yake na mumewe ambaye alianza kumcharaza bakora mpaka alipopoteza maisha.

Kamanda Mpinga alisema kuwa baada ya kusababisha mauaji hayo, Shilondi alikimbia na hajulikani alipo na kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Ifisi wakati Jeshi la Polisi likiendelea kumsaka mtuhumiwa.

Katika tukio lingine, Kamanda Mpina alisema mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Florian Kagombe (46), mkazi wa kijiji cha Itumbi wilayani Chunya aliuawa na walinzi wa Kampuni ya Itumbi Reaching Plant inayojishughulisha na uchenjuaji wa dhahabu baada ya kudhaniwa kuwa ni mwizi.

Taarifa hiyo iliwataja waliofanya mauaji hayo kuwa ni Imani Kayuni (36) na Kelvin Ngonyani (32) wote walinzi wa Kampuni ya Panic Security Group ambao wanadaiwa kumshambulia Kagombe kwa kumpiga na vitu vibutu mpaka kupelekea umauti.

Inadaiwa kuwa watuhumiwa walipomkuta Kagombe katika eneo la kampuni hiyo majira ya saa 2:00 usiku mwishoni mwa wiki, walimshuku kuwa ni mhalifu hivyo wakamshambulia na kisha wakamwachia akiwa taabani.

Hata hivyo ainadaiwa marehemu alipoteza maisha majira ya saa 9:00 alasiri juzi kijijini hapo na kwamba mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Watuhumiwa wawili hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, taarifa ilisema.

Aidha, Kamanda Mpinga alitoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo mtuhumiwa wa mauaji ya Minza kutoa kwa jeshi hilo, ili kufanikisha kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)