MAALIM SEIF AMPA PONGEZI MAGUFULI

Admin
By -
2 minute read
0
KWA mara ya kwanza, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kwa kuiongoza nchi vizuri kwa mwaka uliopita wa 2017.

Maalim Seif alitoa pongezi hizo jana, nyumbani kwake Mbweni mjini Zanzibar akisema kuwa Rais Magufuli amejitahidi katika udhibiti rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Alisema kuwa Rais Magufuli amefanya juhudi za udhibiti wa madini, ili Watanzania wanufaike na rasilimali za nchi.

Alisema kuwa serikali inayoongozwa na Rais Magufuli imechukua hatua pia katika suala la makinikia na limeleta faida kwani kiwango kikubwa cha fedha zingeweza kupotea.

Alisema ingawa bado rushwa haijaisha kabisa, lakini Magufuli amejitahidi na imepungua kulinganisha na uongozi wa awamu ya nne ambapo rushwa ilikithiri.

“Kweli Magufuli amepambana na rushwa na amepambana na mapapa na vidagaa katika rushwa na ameimarisha nidhamu ya nchi, kwani fedha nyingi zilikuwa zikitumika kuwalipa wafanyakazi hewa,” alisema Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF mwaka 2015.

Aliongeza kwa kusema: “Utawala wake wa awamu ya tano kwa mwaka 2017 kuna mazuri ambayo ameyafanya na sisi wanasiasa tusione tabu kuyasema mazuri yake.”

Aidha, alisema kuwa licha ya mazuri hayo, lakini watawala nao wasione tabu wanapokosolewa wanatakiwa wavumilie

Alisema pia Rais Magufuli amejitahidi katika suala la ajira kwa vijana bila ya ubaguzi, hivyo ni vyema hatua kama hizo zikachukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Katibu Mkuu huyo alimtakia mafanikio zaidi Rais Magufuli katika kuiongoza Tanzania kwa mwaka 2018 na kuendelea kuimarisha umoja, upendo na amani ya nchi.

Akizungumzia changamoto katika mwaka 2017, Maalim Seif alisema kuwa uhuru wa vyama vya siasa umebanwa kutokana na kupigwa marufuku mikutano ya hadhara na maandamano.

Alisema kwa upande wa Zanzibar ubaguzi umekithiri na kuwa ajira zinatolewa kwa itikadi za kisiasa na sio kwa sifa au uwezo wa mtu.

“Huwezi kuendesha nchi kwa ubaguzi au kwa itikadi za kisiasa,” alisema Maalim Seif na kusisitiza kuwa Zanzibar iuige utaratibu wa Rais Magufuli katika kuiongoza nchi.
Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)