Uamuzi wa rais Donald Trump wa kumuua Qasem Soleimani, Jenerali wa vikosi vya Qudsi vinavyoungwa mkono na Iran umesababisha msururu wa maafa ambayo yameanza kushuhudiwa.
Kwanza ni vita ambavyo havikukamilishwa vya kupambana na makundi ya jihadi.
Mara mauaji hayo yalipotokea, muungano unaoongozwa na Marekani wenye kukabiliana na kundi la Islamic State ulisitisha oparesheni zake nchini Iraq.
Marekani na washirika wake walitangaza kwamba kazi yao kuu ilibadilika na kuwa kujilinda.
Kwa mtazamao wa kijeshi, bila shaka hawakuwa na cha kufanya zaidi ya hilo.
Iran na vikosi ambavyo inaviunga mkono hapa Iraq wameapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya Qasem Soleimani yaliyosababishwa na bomu lililorushwa na ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani, iliyolenga gari la Soleimani wakati linaondoka uwanja wa ndege wa Baghdad Ijumaa iliyopita.
Hatua hiyo inaweka vikosi vya Marekani vilivyopo Iraq na vile vya washirika wake wa nchi za Magharibi kujumuishwa kwenye vita hivyo.
Na pia hiyo ni hatua itakayofurahiwa na kundi la Islamic State ambalo litafanikiwa kujiimarisha tena kwa haraka baada ya utawala wake kuangushwa.
Pia ni habari njema kwa wenye msimamo mkali kwamba bunge la Iraq lilipitisha muswada unaotaka raia wa Marekani kuondoka mara moja kote nchini humo.
Chimbuko la kundi la IS ni kundi la al-Qaeda nchini Iraq lililosambaratika na limekuwa imara kwa miaka mingi.
Operesheni kubwa ya kijeshi mwaka 2016 na 2017 ilihitajika ili kumaliza utawala wa kundi la IS nchini Iraq na Syria.
Wapiganaji wengi wa Jihadi waliishia kufa ama kuwa wafugwa lakini hilo halikufanikiwa kusambaratisha kabisa kundi hilo.
Na ukweli ni kwamba kundi la IS bado ni imara katika maeneo ya Iraq na Syria ambako limesababisha uvamizi, ubadhirifu wa fedha na vifo kwa wengi.
Nchi ya Iraq ina jeshi na vikosi vya polisi bora waliopewa mafunzo na Marekani na washirika wa Ulaya waliojiunga katika vita dhidi ya IS.
Tangu mauaji ya Soleimani, Marekani imesitisha mafunzo yake pamoja na operesheni zake ikiwa ni pamoja na Denmark na Ujerumani.
Ujerumani inaondoa wanajeshi wake waliokuwa wanatoa mafunzo nchini Jordan na Kuwait.
Vikosi vya Iraqi ndivyo vyenye kuwa katika hatari zaidi wakati wa oparesheni ya ardhini dhidi ya IS.
Lakini pamoja na mafunzo pia vimekuwa vikitegemea pakubwa usafiri kutoka kwa vikosi vya Marekani ambavyo kwa sasa vinanyemelea ngome yao.
Wanamgambo wa IS wana jambo la kusheherekea. Wakati Trump ameamua kumuua Soleimani huo ulikuwa ushindi mkubwa kwao baada ya Marekani kumuua mmoja ya adui zake.
Mwaka 2014, wanamgambo wa Jihadi walianza kufanya mashambulizi na kutwaa maeneo muhimu ya Iraq ikiwemo mji wa pili kwa ukubwa wa Mosul.
Ayatollah Ali al-Sistani, kiongozi wa kidini wa Kishia wa Iraq, alitoa wito wa kujihami kukabiliana na Wasunni wenye msimamo mkali.
Na maelfu ya vijana Wakishia wakajitokeza na kujitolea na kwa ushirikiano na Soleimani na kikosi chake cha Qudsi, walikuwa sehemu ya mabadiliko makubwa katika vikosi vya jeshi. Wanajeshi hao walikuwa wenye nguvu na uwezo mkubwa wa kukabiliana na IS.
Kwa sasa, makundi yenye kuungwa mkono na Iran yamejumuishwa kwenye jeshi la Iraq chini ya muungano unaojulikana kama Popular Mobilisation. Viongozi wa vikosi hivyo wamekuwa viongozi wa kisiasa wenye madaraka makubwa.
Baada ya 2014, Marekani na vikosi hivyo walikabiliana na adui mmoja. Lakini vikosi vya Kishia kwa sasa vinaonekana kuwa na uhakika wa kurejejelelea ajenda yao ya awali ambayo ni kukabiliana na muungano unaoongozwa na Marekani baada ya kuvamiwa mwaka 2003.
Wakati huo, waliwaua wanajeshi wengi wa Marekani - baada ya kupewa mafunzo na silaha zilizowasilishwa na Soleimani moja ya sababu iliyopelekea Trump kutoa agizo la kuuawa kwake wiki iliyopita.
Tangu Trump alipoamua kujiondoa kwenye makubaliano ya mwaka 2018, uhusiano wa Marekani na Iran umezorota zaidi na kuonekana kutafutana vita.
Kabla ya Soleimani kuuawa vikosi vya Shia vilikuwa wameanza kulenga Marekani.
Shambulizi lililotokea mwishoni mwa Disemba katika kambi ya jeshi kaskazini mwa Iraq na kusababisha kifo cha mkandarasi wa Marekani, kulijibiwa kwa mashambulizi ya anga yaliyosababisha vifo vya wapiganaji karibia 25 wa kundi la waasi la Kataib Hezbollah.
Kiongozi wao Abu Mahdi al-Muhandis, alikutana na Soleimani uwanja wa ndege wa Baghdad na walirushiwa bomu wakiwa kwenye gari moja.
Historia inaonesha kwamba makundi ya jihadi yenye msimamo mkali hujiimarisha zaidi wakati kunapokuwa na ukosefu wa uthabiti, mapigano na kudhoofisha maadui zao ambao kipindi hicho huwa wamegawanyika.
Hilo limewahi kutokea na kuna uwezekano mkubwa kwamba litatokea tena.