Emily Mugeta, Mtanzania Anayewasumbua Ujerumani

Admin
By -
0
EMILY Mugeta safari yake ya soka ilianza akiwa kwenye Kituo cha TSC kilichopo mkoani Mwanza. Mwaka 2012, akaanza kufahamika zaidi akiwa na timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.

Mugeta mwenye uwezo wa kucheza beki wa kushoto, anasema mwaka 2012 TSC ilipata mwaliko wa kwenda kushiriki michuano maalum nchini Ujerumani, akaenda nayo.

Mwenyewe anasema safari hiyo ndiyo ilifungua milango ya kuwepo nchini Ujerumani hadi leo hii licha ya wakati alipotakiwa kuelekea nchini humo kushiriki michuano ya Inzel Cup, Kocha wa Ngorongoro, Kim Poulsen wakati huo alimgomea kutokana na kuwepo katika mipango yake ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia chini ya miaka 20.

Mugeta amefanya mahojiano kwa kina na Spoti Xtra, hapa anaanza kufunguka: “Haikuwa kazi rahisi kwa kuwa Kim hakuwa anataka niende Ujerumani, lakini niliweza kwenda kwa ruhusa.
“Ujerumani tuliweza kukutana na timu nyingi kama vile TSV 1860 Munich, Maccabi Haifa na TSG 1899 Hoffenheim, lakini kwa bahati mbaya tuliishia robo fainali.
“Kitu kizuri baada ya hapo, nilifanikiwa kupata mwaliko wa kwenda kufanya majaribio kwenye Klabu ya Maccabi na wakati ule ilikuwa ikishiriki Europa League.
“Kwa bahati mbaya sikuweza kwenda kutokana na kutokea mgogoro kati ya yule Mzungu aliyefanikisha timu yetu ikaenda Ujerumani na wamiliki wa kituo kilichonilea, dili likafa.

“Nikarejea Tanzania moja kwa moja kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes, Kocha Kim akawa amechukia kwa sababu nilizidisha siku wakati nipo Ujerumani, sikuweza kusafiri kwenda kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Nigeria. Kumbuka mechi ya kwanza hapa nyumbani tulifungwa.

“Baada ya hapo, nikarejea Simba ambapo nilikuwa nacheza kwa mkopo nikitokea TSC, lakini wakati huo kuna mtu kule Ujerumani nilikuwa nawasiliana naye ambaye alikuwa kwenye yale mashindano akifuatilia na alinieleza anataka kunisaidia kwa kuwa nina kipaji.

“Bahati mbaya kwamba sheria za Ujerumani zinahitaji mchezaji akienda kule moja kwa moja akacheze Bundesliga, sasa jambo la kupindisha sheria kwa wenzetu ni gumu sana.

“Nashukuru wakati tulipokuwa kule Ujerumani kuna mtu nilikuwa naye halafu tayari alikuwa na mtoto wangu, hilo ndilo jambo ambalo lilinisaidia kwa sababu nilimwambia, akanisaidia.
“Yule jamaa aliwasiliana na yule mama mtoto wangu, kuna barua akampatia ili aweze kuthibithisha ili niweze kwenda Ujerumani.

“Kipindi hicho Kocha wa Simba, Patrick Liewig akawa amenipandisha kwenye timu ya wakubwa, alipokuja Zdravko Logarusic, kukatokea kama mvurugano, watu wengi wakaondoka.
“Mimi nikajiunga na Polisi Moro kwa ajili ya kujiweka sawa wakati nasubiria mchongo wa kwenda Ujerumani kwa mara nyengine.

“Mara ya pili nilienda Ujerumani mwaka 2015, baada ya kufika kule yule mtu ambaye alikuwa akinifuatilia ndiyo alikuwa nyuma yangu katika kutafuta timu, nikapata timu ya Neckarsulmer SU iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Tano.

“Lakini mwishoni mwa msimu nilipata jeraha la bega, nikakaa nje msimu mmoja na miezi mine, ila baada ya kupona niliachana na ile timu, nikajiunga na Sportfreunde Lauffen.

“Nashukuru nikiwa hapo niliweza kufanya vizuri na wakati huo Fenerbahce wakawa wanifuatialia hadi tukawa tumeanza mazungumzo ya kwenda kufanya majaribio.
“Tulikubaliana na watu kwamba watakuja kuniona wakati nacheza maana awali waliniona kupitia mtandao.
“Kabla ya wao kuja, kulikuwa na mechi tulitakiwa kucheza, kisha wao waje inafuata. Sasa katika hiyo mechi kabla ya hao jamaa hawajaja kuniona, dakika kama ya 70 hivi nilikuwa nawania mpira na mchezaji wa timu pinzani.

“Katika kuwania kule mpira, tukapiga kibuyu ambacho kilisababisha mwenzangu aanguke chini, mimi nikawa naendelea na mpira.
“Lakini cha ajabu mwamuzi alikuja kunipa kadi nyekundu ambayo kwa sheria zao unatakiwa kukaa nje kwa wiki nne.

“Mbaya zaidi lile tukio mwalimu wa timu yangu likamkera, akaniongezea adhabu ya mechi nne halafu akanitaka mazoezi nifanye na timu ya pili.
“Sasa nikawa na adhabu mbili, moja ya ligi ambayo ni ya kukaa nje wiki nne na nyingine ni ya kocha kuniondoa kwenye kikosi.
“Kiukweli ulikuwa wakati mgumu sana kwangu kwa sababu watu wa Fenerbahce kutoka Uturuki walikuwa wanakuja kuniangalia kwenye mechi ijayo kutokana na makubaliano yetu ila mambo yakawa yameharibika,” anasema Mugeta.

Unajua nini kilitokea kuhusiana na dili lake la kwenda kufanya majaribio Fenerbahce? Usikose Spoti Xtra Jumapili katika mwendelezo wa makala haya.
Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)