CHADEMA WAFUNGUKA KUHUSU MANGE KIMAMBI

Admin
By -
0
WAKATI afya ya Tundu Lissu ikiendelea kuimarika, Yasinta Massawe ndiye ameongoza kundi la watu walio ughaibuni kutoa kiasi kikubwa zaidi cha fedha kusaidia matibabu ya mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema).

Kwa mujibu wa mtandao wa https://www.gofundme.com/Lissumedicalcare, hadi jana alasiri jumla ya Dola za Marekani 33,077 (Sh. milioni 72.3) zilikuwa zimepatikana kutokana na michango ya watu 705 walio ughaibuni walioitikia wito na kampeni zinazofanywa na Chadema na marafiki wa chama hicho kusaidia matibabu ya mbunge huyo.

Mtandao huo ulionyesha kuwa hadi muda huo, mwanamama huyo alikuwa kinara akichangia Dola za Marekani 3,000 (Sh. milioni 6.6). Alichanga miezi miwili iliyopita.

Yasinta alifuatwa na Nyau Mwinyi aliyechangia Dola 1,500 (Sh. milioni 3.3), Alexis Bisangwa Dola 500, Stanley Lucas Dola 400, Kelvin Assey Dola 300 na Olotumi Laizer Dola 250.

Kampeni hiyo ya marafiki wa Chadema na Lissu walio nje kusaidia matibabu ya mbunge huyo ilianzishwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji Septemba 12, ikiwa ni siku tano baada ya mtaalamu huyo wa sheria kushambuliwa kwa kupigwa risasi.

Oktoba 17, wakati Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuzungumzia hali ya afya ya Lissu, alisema kiasi cha fedha kilichokuwa kimepatikana hadi Oktoba 12 kutokana na michango ya wadau waliopo ughaibuni kilikuwa Dola za Marekani 29,700 (Sh. milioni 64.9).

"Wapo Watanzania kwenye anga ya kimataifa walichangia fedha Dola za Marekani 29,700 ambapo dada zetu kina Mange Kimambi walisaidia kuhamasisha kupitia mitandao," Mbowe alisema siku hiyo.

Lissu (49), anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi, Kenya baada ya kupigwa risasi tano na watu wasiojulikana akiwa kwenye gari lake nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba 7, mwaka huu. Jumla ya risasi 32 zilirushwa na watu hao kwa mujibu wa taarifa za Bunge.

Wiki iliyopita familia ya mbunge huyo ilieleza kuwa afya yake inazidi kuimarika na anatarajiwa kuondolewa hospitalini hapo na kupelekwa nje ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuanzishiwa mazoezi ya viungo.

Katika mkutano wake wa Oktoba 17, Mbowe alisema kuwa hadi Oktoba 12, Mwanasheria huyo wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS) alikuwa amefanyiwa operesheni 17 na matibabu yake yalikuwa yamegharimu Sh. milioni 412.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia alisema Lissu alikuwa ametumia kiwango kikubwa cha damu kuliko wagonjwa wengine wote waliowahi kutibiwa kwa miaka 20 iliyopita katika Hospitali ya Nairobi.

Katika mchanganuo wa matumizi ya fedha, Mbowe alieleza siku hiyo kuwa gharama zilizotumika tangu alipolazwa Septemba 7 hadi Oktoba 12 zilikuwa Sh. milioni 412.47.

Alisema kiasi hicho cha fedha kimetokana na michango ya wadau mbalimbali wakiwamo wanachama, wabunge, ndugu, marafiki kutoka ndani na nje ya nchi na wafanyabiashara wadogo na kati ambao wamesaidia kwa kiwango kikubwa matibabu hayo.

“Tumepokea michango mingi ambayo imewezesha kwa kiwango kikubwa kusaidia matibabu ya Mheshimiwa Lissu. Kundi la kwanza katika kuchangia ni wabunge wa Chadema ambao walichanga Sh. milioni 48.4," Mbowe alisema.

"Wananchi na viongozi wengine wa chama walichanga Sh. milioni 24.2, wanachama na viongozi na familia walichanga kupitia akaunti maalum ya CRDB Sh. milioni 90.8, michango iliyochangwa na wabunge wote Sh. milioni 43."

Alisema Watanzania kwenye anga ya kimataifa walikuwa wamechangia Dola za Marekani 29,700 huku akibainisha kuwa jopo la madaktari 12 ambao walikuwa wanamtibu Lissu walilipwa Dola za Marekani 46,440 kufikia Oktoba 12 kwa kuwa kila daktari anapotoa huduma kwa muda fulani anahitajika kulipwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi iliyopita, kaka wa Tundu Lissu, wakili Alute Mughwai alisema, taratibu za kumsafirisha nje ya nchi zimeanza.

KUFANYA MATAMBIKO
“Awamu ya tatu ya matibabu yake ni muhimu sana kwani itahusu pia mazoezi ambayo kama haitafanyika vyema ataweza kupata ulemavu wa kudumu,” alisema Mughwai.

Mughwai alisema alizungumza na Lissu Nairobi na alimweleza kuwa akirejea nchini atakwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuwashukuru madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Mkoa kwa kuokoa maisha yake siku aliyopigwa risasi.

Wakili Mughwai alisema Lissu amemwambia baada ya hapo atakwenda kanisani na msikitini kumshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yake kwa kufanya ibada maalumu.

“Baada ya ibada, tutaangalia utaratibu kifamilia kama itawezekana kwenda kufanya matambiko kwenye makaburi ya wahenga wetu 76 waliofariki katika vita miaka 200 iliyopita,” alisema.

Alisema baada ya hapo, Lissu anatarajia kuendelea kufanya kazi zake za siasa na uwakili pale alipoishia kwa ari kubwa.


Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)