TAKUKURU YATANGAZA KUTOA MILIONI KUMI KWA ATAKAE SAIDIA KUMPATA MWASIBU ALIYE KIMBIA
By -
November 14, 2017
0
Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza donge nono la Sh10 milioni kwa yoyote atakayefanikisha kukamatwa kwa aliyekuwa mfanyakazi wake Godfrey Gugai.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Novemba 14, Naibu Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo amesema Gugai anatuhumiwa kujipatia mali nyingi kinyume cha Sheria ya Utumishi wa Umma.
Amesema kwa nafasi ya Gugai ya mhasibu wa taasisi hiyo ni vigumu kupata mali nyingi kiasi hicho.
"Awali tulipomhoji alitoa ushirikiano lakini tukiwa tunaendelea alitoweka na kwa taarifa tu amekuwa akitoka kwa magendo nje ya nchi, kwa yeyote atakayefanikisha kumpata tutamzawadia Sh10 milioni," amesema Mbungo
Amesema baada ya kutoweka walikwenda mahakamani kuhusu mali zake na tayari kuna zuio la kutokufanya kitu chochote yaani visiuzwe au kuendelezwa.
Amezitaja baadhi ya mali anazomiliki mikoa mbalimbali ni nyumba zaidi ya tano, viwanja zaidi ya 30 na magari matano.
"Kama atakuja na kutupa ushirikiano ikiwamo kuthibitisha uhalali wale basi tutamwachia mali yake lakini kwa nafasi yake kumiliki mali zote hizi zinatutia walakini," amesema
Naibu mkurugenzi huyo amewaonya watumishi wa umma kutokutumia vibaya madaraka yao waliyopewa kwani wakibainika hawatasita kuwachukulia hatua.
Tags: