Header Ads Widget

RAIA WA KENYA MWENYE HIV ASHANGAZA WATU


 

Susan Metta ni mwanamke wa miaka 40 kutoka nchini Kenya. Miaka minne iliyopita alipopashwa habari za kuwa alikuwa na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi,badala ya kukumbwa na simanzi huzuni na machungu, mwanadada huyu anasema kuwa alitabasamu tu na kumueleza muhudumu wa afya aliyekuwa naye kuwa ampatie dawa za kupunguza makali ya HIV yaani ARVS.

"Nakumbuka tarehe 16 Januari 2019 siku niliyojipatia nguvu kufika hospitalini kupimwa virusi vya ukimwi baada ya kuugua kwa karibu miezi sita. Kwa hiyo matokeo yalipoletwa mimi niliridhika kwani kati ya HIV na saratani mimi nilikuwa nahofia saratani zaidi," anasema Metta .

Mwanadada huyu anasema kuwa dalili alizokuwa nazo kabla ya kupimwa zilikuwa zinaashiria uwepo wa saratani kulingana na uzoefu na alichokielewa kuhusu maradhi hayo .

Chanzo cha maambukizi

Susan Metta anapofikiria kuhusu safari yake ya kugundua kwamba alikuwa mwathiriwa wa HIV anashuku alipata maambukizi kati ya mwaka wa 2016-2017 .

Susan Metta

CHANZO CHA PICHA,SUSAN METTA

Maelezo ya picha,

alikuwa na mahusiano ya kiholela ya mapenzi , hali inayofanya kuwa vigumu kunyoosha kidole cha lawama kwa mwanamume mmoja

IIjapokuwa hana uhakika ni nani haswa aliyemuambukiza, amekiri kuwa kabla ya kukutana na mpenzi wake ambaye walikuwa wanaishi naye wakati huo nchini Kenya, alikuwa na mahusiano ya kiholela ya mapenzi, hali inayofanya kuwa vigumu kunyoosha kidole cha lawama kwa mwanamume mmoja.

Hata hivyo anasema kuwa kwa wakati huo alikuwa amekaa kwa muda na mpenzi waliyekuwa naye.

"Kati ya kipindi nilichopashwa taarifa kuwa nilikuwa nimeambukizwa virusi HIV na wakati ambao nashuku niliambukizwa huenda ilikuwa miaka kadhaa,'' alisema.

''Iwapo muathiriwa anakula vizuri na haishi maisha ya ulevi na msongo wa mawazo , virusi vya HIV huwa vinatulia ndani ya mwili .Kwa hio nadhani hicho ndicho kilinifanya kufahamu hali yangu kuchelewa,"anakumbuka Metta.

kipindi hicho cha 2018 ndipo alianza kuhisi mabadiliko katika mwili wake.

CHANZO CHA PICHA,SUSAN METTA

Maelezo ya picha,

kipindi hicho cha 2018 ndipo alianza kuhisi mabadiliko katika mwili wake.

Bi Metta anasema kuwa kati ya mwaka 2008 hadi mwaka wa 2018 alikuwa anafanya kazi za mikataba nchini Sudan Kusini , alikuwa na kazi nzuri ya kusimamia baadhi ya mikahawa mikubwa mjini Juba katika kipindi hicho .

Ila anasema kuwa kipindi hicho cha mwaka wa 2018 ndipo alianza kuhisi mabadiliko katika mwili wake.

"Mara nilikuwa nahisi ghafla nina homa , mara nahisi baridi au joto la kupindukia, lakini kwa kuwa nilikuwa nchi ya kigeni ambapo joto ni jingi nilidhania kuwa ni jambo la kawaida kuathiri mwili wangu"anaongezea

Juni 21, 2018 mwanadada huyu aliwasili katika uwanja wa ndege wa mjini Juba Sudan Kusini kutumikia mkataba mwengine kama ilivyokuwa ada yake.

Mwanamke huyu anasema kuwa alihudumu kama meneja na kusimamia utendakazi wa watu.

Anasema kwamba ni kazi aliyoifanya kwa ari kubwa.

Nyumbani Kenya alikuwa amemuacha mpenzi wake ambaye walikuwa wanaishi nyumba moja .

Dalili za mwili wake kuwa na ugonjwa zilianza pindi alipofika nchini Kenya

CHANZO CHA PICHA,SUSAN METTA

Maelezo ya picha,

Dalili za mwili wake kuwa na ugonjwa zilianza pindi alipofika nchini Kenya

Alifanya kazi yake mwezi Juni hadi mwezi Septemba wakati walipofutwa kazi ghafla na mikataba yao kufika kikomo bila notisi.

Anakumbuka kwamba wakati huo alizongwa na msongo wa mawazo uliomfanya kutumia pombe mara kwa mara kinyume na kawaida yake .

Dalili za mwili wake kuwa na ugonjwa zilianza pindi alipofika nchini Kenya , alihisi homa na kikohozi ambacho hakikuwa na tiba licha ya kunywa dawa kila wakati .

Vilevile uhusiano wake na mpenzi wake ulikuwa na misukosuko na ulikuwa unayumba mno.

"Nilipofika nyumbani, tulikuwa tunakosana mno na yule mpenzi wang , kwanza nilikuwa na mawazo kuhusu kusimamishwa kazi ghafla, pili nilikuwa nimezoa maisha ya kuwa na pesa zangu na sasa ilibidi nianze kuzoea maisha ya kupewa na huyu mtu. Hapo ndipo maisha yalianza kuwa changamoto kwa kiasi cha afya yangu kuanza kuathirika."

Haikuchukua muda kwa Bi. Metta kuamua kuhama na kuanza maisha ya kuishi pekee kwani uhusiano wake na mpenziwe uliendelea kuwa na kero.

Alipoanza kuishi peke yake hapo ndipo afya yake ilidorora kwa kiasi kuwa ilikuwa wazi kwamba alikuwa na maradhi asiyoyaelewa .

Mwili wake ulianza kubadilika mno kwa mfano anasema kuwa kila siku aligundua kuwa alikuwa anapoteza uzito kwa kasi mno, vilevile muonekano wa rangi ya nywele zake ulianza kubadilika na kuwa na wekundu usio wa kawaida hali kadhalika wingi wa nywele zake ukawa unapungua.

"Jaribio langu la kutibu shida moja kwa mfano kuumwa na kichwa leo, kesho yake nilikuwa na tatizo la kuumwa na tumbo mbali na shida ya homa na joto kali mwilini. kwa hio iliwadia wakati nikaanza kushuku kuwa nilikuwa na gonjwa sugu .Hofu yangu kuu ilijiri nilipopata vidonda katika sehemu ya juu ya mdomo wangu," anakumbuka Metta

Siku ya msema kweli

Januari 14, 2019 alielekea hospitalini akiwa na lengo la kupimwa iwapo alikuwa na virusi vya HIV, Iia alipofika hospitalini aliishiwa na nguvu na mhemko wa yale yaliokuwa mbele na kuamua kurudi nyumbani bila kufahamu ukweli kuhusu afya yake .

Ila siku mbili baadaye tarehe 16 mwaka 2019, Metta aliwaita dada zaake wawili kuandamana naye hospitalini ili kufanyiwa uchunguzi wa HIV .

Alipimwa damu na baada ya muda wa saa tatu matokeo yake yalibaini alikuwa na virusi vinavyosababisha HIV.

CHANZO CHA PICHA,SUSAN METTA

Maelezo ya picha,

Alipimwa damu na baada ya muda wa saa tatu matokeo yake yalibaini alikuwa na virusi vinavyosababisha HIV.

Kulingana na Metta dada zake walipomuuliza ni kwanini aliamua kufanyiwa uchunguzi wa virusi vya HIV, Jibu lake lilikuwa alichoka kuwa na dalili za magojwa madogo madogo mwilini mwake .

Alipimwa damu na baada ya muda wa saa tatu matokeo yake yalibaini alikuwa na virusi vinavyosababisha HIV.

"Nilipopewa matokeo yangu , cha ajabu ni kuwa sikuwa na wasiwasi wala uwoga , nilikuwa nimejitayarisha kwa matokeo kama hayo kulingana na dalili nilizokuwa nazo ''.

Hatahivyo anasema kwamba dada zake waliangulia kilio huku yeye akiwa ametosheka na matokeo hayo,

''Nilifahamu kuwa nitakuwa na dawa za kunisaidia kupigana na makali ya Ukimwi "Metta anasema

Je ni nani aliyemuambukiza?

"Baada ya kupata matokeo , niliamua kumpigia simu yule aliyekuwa mpenzi wangu wa mwisho ili nimpashe matokeo hayo , baada ya kupokea ujumbe huo hakuonyesha dalili za kushtuka, cha muhimu nikuwa alikubali kutembea nami katika safari hii, kwa ufupi mimi siwezi kusema kuwa ni yeye aliyenipatia HIV au la "anasema mwanadada huyo.

Mwanadada huyu anasema kuwa changamoto ya kufahamu ni nani aliyemwambukiza inatokana na yeye kukiri kuwa , kabla ya kukutana na mpenziwe alikuwa katika mahusiano yaliokuwa hayana uangalifu hata kidogo..

Ananongezea kwamba kabla ya uhusiano huo alikuwa kwenye mahusiano mengine ambayo hakujua hali ya watu alioshiriki nao mapenzi .

Susan Metta

CHANZO CHA PICHA,SUSAN METTA

Anasema kwamba hali yake ya kutojali afya na maisha yake ilimtumbukiza katika hali hio .

Ila kwa sasa ana ushauri kwa vijana na watu wote

"Samahani kusema kuwa pengine ni mimi nimeambukiza wengine na wala sio wale niliyokuwa nao , ninachosema ni kuwa tabia ya kutojali kuhusu afya ya mpenzi mwenzako kabla ya kushiriki ngono ndio inatoa nafasi ya kutofahamu kati ya watu uliokuwa nao ni nani aliyehusika. "Metta anasema

Wazo la mwisho

Vile vile mwanadada huyu ambaye kwa sasa ni balozi wa kutetea na kuwakilisha maswala ya watu wanaoishi na HIV na Ukimwi nchini Kenya anasema kuwa :

"Watu waache kupima HIV au Ukimwi kwa macho, usimuone mtu amenona , ngozi nyororo ukadhania hana , huenda yeye ndiye aliyeathirika - Vile vile unapoelezwa una virusi vya HIV usikate tamaa anza matumizi ya dawa kila siku na huenda ukaishi maisha marefu yasio na bughudha", Metta anasema

Susan Metta alianzisha vipindi vya mahojiano katika mtandao wa YOUTUBE kama njia mojawapo ya kuhamasisha jamii kuhusu , pandashuka za watu wanaoishi na virusi vya HIV,

Susan Metta

CHANZO CHA PICHA,SUSAN METTA

Katika mtandao wake utatazama na kusikia simulizi za waume na wanawake ambao wanaeleza changamoto na madhila mengi waliopitia kama waathiriwa.

Bi.Metta anasema kuwa mtandao huo umekuwa nguzo na tiba kwa wengi hasa kutokana na unyanyapaa mwingi unaotokana kwa baadhi ya watu katika jamii kuhusu watu kama yeye .

Post a Comment

0 Comments