Raia wanne wa Uchina wamekamatwa na polisi baada ya video kusambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha raia wa Uchina akimchapa viboko raia wa Kenya.
Inasemekana kwamba raia wa Uchina mfanyakazi wa mgahawa mmoja uliopo mjini Nairobi, alinaswa akimchapa mfanyakazi raia wa Kenya kupitia kamera kwa madai ya kufika kazini akiwa amechelewa.
Jumapili, mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) amesema watu wanne raia wa Uchina wamekamatwa baada ya kuripotiwa kuwa mfanyakazi mmoja wa kenya ameshambuliwa.
Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai Kenya kupitia mtandao wa twitter imeandika,
''Baada ya taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari zinazomuonesha mwanamume mwenye asili ya Asia akimshambulia mwanamume mmoja ambaye inasemekana ni mfanyakazi wa hoteli hiyo, asubuhi ya leo wapelelezi wamefika katika hoteli ya Chez Wou eneo la Kileleshwa kuchunga kisa hicho.''
Wapelelezi wa DCI walifanikiwa kumkamata mshukiwa Deng Hailan, raia wa uchina anayefanyakazi katika hoteli hiyo kama mpishi mkuu lakini hana kibali cha kufanyakazi Kenya.
Wengine waliokamatwa ni raia watatu wa Uchina wanaofanya kazi katika mgahawa huo kwa mahojiano zaidi lakini pia inadaiwa kwamba kuna baadhi yao hawana vibali vya kufanya kazi Kenya ama wameingia kwa visa za utalii.
Pia miongoni mwa waliokamatwa ni Yu Ling, keshia katika hoteli hiyo ambaye ana visa ya utalii lakini hana kibali cha kufanyakazi.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya video kusambaa katika mitandao ya kijamii inayomuonesha raia mwenye asili ya Asia akimchapa viboko mhudumu wa hoteli moja raia wa Kenya katika mgahawa wa Chez Wou uliopo eneo la Kileleshwa, Nairobi wiki iliyopita.
Raia wa kenya wameonesha hasira zao na kudai hatua ya kisheria ichukuliwe.
Aidha, ubalozi wa Uchina Nairobi, umeonekana kuunga mkono hatua iliyochukuliwa na serikali ya Kenya baada ya kuashiria kwamba wameona video ya kuchapwa viboko kwa raia wa Kenya iliyowekwa katika mtandao na runinga ya K24, na kuandika ujumbe ufuatao kupitia mtandao wake wa Twitter.
Jumapili, polisi walivamia hoteli hiyo na kuwakamata wafanyakazi wanane raia wa kenya na raia wanne wa Uchina kwa mahojiano.
Inasemekana kwamba mtu aliyeshukiwa kutekeleza kisa hicho alitakiwa kufika kwenye ofisi za uhamiaji lakini hakufanya hivyo.