Nani atakayeshinda tuzo ya Oscar ya picha bora?
Tutajua kwa hakika pale mshindi atakapojulikana siku ya Jumapili jijini Los Angeles, lakini kuna mafunzo machache kutokana na mazingira ya sherehe zilizotangulia ambazo zinaweza kutupa mwelekeo kiasi.
Kukisia filamu gani itashinda tuzo hiyo kubwa ni kazi ya wapenzi wa filamu, wakosoaji, watunzi wa vitabu hata wataalamu wa hesabu- watu pia wamekuwa wakiandika tafiti kuhusu makisio ya tuzo za Oscar.
Lakini baadhi ya mahitimisho kuhusu namna gani filamu zinaweza kujiongezea nafasi ya ushindi wa picha bora kwenye tuzo ya Oscar inashangaza kidogo.
Urefu wa filamu
Urefu wa filamu ni suala lenye uzito kwenye tuzo za Oscar
Wanaochaguliwa kuwania tuzo ya picha bora na washindi, filamu zao ni ndefu.
Tovuti ya masuala ya burudani, Collider ilikusanya data kutoka kwenye tuzo hizo na kugundua kuwa 59 kati ya washindi 91 filamu zao zilikuwa na urefu wa dakika 120.
Ilibaini kuwa filamu ndefu miongoni mwa zinazoorodheshwa kwa ajili ya kushindanishwa ilikuwa na uwezekano wa kunyakua tuzo.
Kutazamwa sana kwa filamu hakumaanishi ushindi
Mafanikio mazuri kwenye majumba ya sinema hayamaanishi ushindi, au sifa ya kuingia kwenye tuzo za Oscar.
Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, filamu tatu pekee zilizoshinda tuzo ya picha bora pia ilikuwa kwenye chati za juu miongoni mwa filamu zilizokuwa zikitazamwa na wengi kwenye nyumba za sinema, nazo ni Rain Man (tuzo za Oscar 1989), Titanic (1998) na Lord of The Rings: Return of the King (2004).
Kwa hakika hakuna miongoni mwa washindi tangu mwaka 2004 waliokuwa kwenye orodha ya kumi bora ya filamu zilizotengeneza pesa nyingi kwa mwaka ambao filamu hizo zilitolewa.
Mwaka huu filamu pekee ambayo inaweza kuvunja msimamo huo Joker, ambayo ilitolewa mwaka 2019, ilikuwa filamu ya saba kwenye orodha ya filamu zilizoingiza fedha nyingi.
Tengeneza filamu aina ya Tamthilia
Tamthiliya ni aina ya filamu zinazofanikiwa katika historia ya tuzo za Oscar.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa data za Academy, filamu zilizoshinda 47 miongoni mwa 91 ni tamthiliya, ucheshi ni ya pili kwa kuwa filamu zake 11 zilishinda.
Siku hizi bajeti yako haifanyi filamu yako ishinde Oscar
Bajeti kubwa katika utengenezaji wa filamu kunaweza kufanya filamu ishinde, lakini kwa sasa hali haiko hivyo mara nyingi.
Ben-Hur, ilikuwa filamu iliyotengenezwa kwa fedha nyingi kuliko zote, ikaweka rekodi kushinda tuzo 11 za Oscar (ikiwemo picha bora) mwaka 1960.
Bajeti yake ilikuwa dola za Marekani milioni 130, zaidi ya mara 25 ya gharama ya filamu ya Moonlight, iliyoshinda Oscar mwaka 2017.
Na sasa filamu ambazo hazijatumia fedha nyingi kama Moonlight zimekuwa zikishinda katika miaka ya karibuni: tangu mwaka 1991 ni filamu ya Titanic (1998), Gladiator (2001) na The Departed (2007) zilikuwa filamu ghali zilizochaguliwa kushinda tuzo.
Ni muhimu kufanya vizuri kwenye tuzo nyingine
Msimu wa Oscar huja baada ya mfululizo wa tuzo kama Golden Globes. Na zote huwa na washiriki ambao pia huweza kuchaguliwa kushiriki tuzo za Oscar.
Hivyo ushindi kwenye tuzo nyingine hutoa picha ya jinsi gani filamu inaweza kufanya vyema kwenye tuzo za Oscar.
Usiwe na muongoza filamu mwanamke
Huu ni ukweli wenye bahati mbaya kwenye tuzo za Oscar. Filamu 12 zilizoongozwa na wanawake ndizo zilizochaguliwa kushindania tuzo ya picha bora - kati ya 560 zilizochaguliwa kwenye historia ya tuzo za Oscar.
Na katika hizo moja pekee- Hurt Locker mwaka 2010-ilishinda.
Mwaka huu 2020, filamu ya Little Women iliyoongozwa na Greta Gerwig imechaguliwa kwenye kinyang'anyiro cha picha bora lakini hakuna mwanamke aliyewahi kushinda kipengele cha muongozaji bora.
Zungumza Kiingereza
Mbali na sifa zinazotolewa na wakosoaji - tuzo kama vile Palm D'Or na tamasha la filamu la Cannes - Filamu ya Korea Parasite imesababisha kuwepo maoni tofauti katika tuzo za mwaka huu kwa sababu inaweza kuweka historia.
Imechaguliwa katika kipengele cha picha bora pia muongozaji filamu bora.
Lakini jambo la kipekee ni kuwa hakuna filamu yeyote isiyokuwa ya lugha ya kiingereza iliyowahi kushinda tuzo hii.
Je mwaka huu sheria hiyo ya ''lugha ya kiingereza'' itavunjwa?