Afrika ni moja ya mabara mwili ambayo bado hayajathibitisha kisa chochote cha virusi vya corona ingawa wataalamu wameonya kuwa hilo huenda lisiendelee kwa kipindi kirefu kwasababu ya uhusiano wa bara hilo na China.
Karibia watu 565 wameaga dunia huku visa vingine zaidi ya 28,000 vikithibitishwa kote duniani, idadi kubwa ikiwa ni kutoka China.
Wiki iliyopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kwamba mlipuko wa virusi vya corona ni ugonjwa wa dharura kwa dunia nzima kwasababu ya hofu kwamba nchi maskini huenda zikashindwa kukabiliana na mlipuko huo.
"Sababu kuu ya kutambua virusi hivi kama hali ya hatari duniani sio Uchina, lakini kile kinachotokea katika nchi zingine. Wasiwasi wetu mkubwa ni uwezo wa kusambaa kwa virusi hivyo, katika nchi zenye mfumo dhaifu wa afya," amesema mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, kutoka Ethiopia.
Mifumo ya afya katika nchi nyingi za Afrika tayari inakabiliwa na ugumu wa kazi zilizolimbikizana, na hapo ndipo tunapojiuliza, je nchi hizi zinaweza kukabiliana na mlipuko kama huu ambao unasambaa kwa haraka mno?
Michael Yao, Mkuu wa huduma za dharura eneo la Afrika, amesema "baadhi ya nchi za Afika sio kwamba hazina pa kuanzia lakini uwezo ni mdogo sana".
"Tunajua vile mfumo wa afya ulivyo dhaifu katika bara la Afrika na mifumo hii tayari inazidiwa na milipuko ambayo inaendelea kujitokeza, kwa hiyo kwetu sisi ni muhimu kuutambua mapema kama janga ili tuweze kudhibiti usambaaji wake."
Ni vifaa gani vilivyopo kwasasa vya kukabiliana na mlipuko wa virusi hivi?
Hadi mapema wiki hii, kulikuwa na maabara mbili pekee zenye uwezo wa kuchunguza virusi hivi barani Afrika - Senegal na Afrika Kusini - zenye vifaa maalumu vinavyohitajika wakati wa kuchunguza virusi hivyo.
Maabara hizo zimekuwa zikitumika na nchi nyingine katika eneo hilo.
Moja ya maabara hizo, Institut Pasteur de Dakar, nchini Senegal kwa kipindi kirefu imekuwa mstari wa mbele katika ubunifu wa tiba Afrika ikiwemo utafiti wa homa ya manjano.
Hata hivyo wiki hii, Ghana, Madagascar, Nigeria na Sierra Leone zimetangaza kwamba pia nazo zina uwezo wa kufanya vipimo vya virusi vya corona.
WHO pia inatuma vifaa vya maabara 29 barani humu kuhakikisha zina uwezo wa kukabiliana na virusi hivyo na pia zisaidie katika kupima visa vitakavyojitokeza ili kuthibitisha iwapo virusi hivyo vipo kwa ajili ya nchi zingine zenye uhitaji.
Hata hivyo, shirika hilo lina matumaini kwamba kufikia mwishoni mwa mwezi huu karibu nchi 36 za Afika zitakuwa na vifaa stahiki vya kupima virusi vya corona.
Uwezo wa nchi za Afrika kupima na kutambua virusi hivyo "unategemea vifaa maalumu vinavyotoka China na Ulaya," amesema Daktari Yao.
Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Nigeria lina watu milioni moja wa kujitolea ambao wako tayari kulisaidia iwapo kutatokea chochote.
Katibu mkuu wa shirika hilo Abubakar Ahmed Kende amesema hatua hiyo inanuia kuzuia uwezekano wowote wa kusambaa kwa virusi hivyo nchini humo na pia kudhibiti mlipuko wa homa ya Lassa ambayo visa vyake vinazidi kuogezeka kote nchini humo.
Nchini Tanzania, Waziri wa afya Ummy Mwalimu alitangaza kwamba vituo vimetengwa kaskazini, mashariki na magharibi mwa nchi hiyo kukabiiana na virusi hivyo. Pia vipima joto vimewekwa tayari huku wahudumu wa afya zaidi ya 2,00o wakipewa mafunzo.
Nchi kadhaa zikiwemo Kenya, Ethiopia, Ivory Coast, Ghana na Botswana zimekabiliana na visa vilivyoshukiwa kuwa vya virusi hivyo, na kuwaweka wahusika kwenye karantini wakati vipimo vyao vya damu vinafanyiwa uchunguzi.
Hatahivyo hadi kufikia sasa vipimo vyote vilivyochunguzwa hakuna kilichothibitika kuwa na virusi hivyo.
Wizara ya afya ya Uganda imethibitisha kwamba ilikuwa imewawekwa watu zaidi ya 100 kweye karantini waliowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe.
Baadhi ya watu hao wamewekwa katika karantini kwenye hospitali mbili mjini Entebbe na Kampala, huku wengine wakiombwa kusalia majumbani.
Je kuna mafunzo yoyote kutokana na ugonjwa wa Ebola?
Daktari Yao alihusika katika milipuko ya Ebola magharibi mwa Afrika 2014-2016 na wa hivi karibuni zaidi ukiwa ule uliotokea Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Alisema ana wasiwasi kwamba Afrika haina uwezo wa kutosha kutibu watakaothibitishwa kuwa virusi vya corona.
"Tunashauri nchi angalau kuwa na uwezo wa kubaini virusi hivyo mapema kuzuia kusambaa kwa virusi vipya ndani ya jamii - jambo ambalo litafanya iwe vigumu kuudhibiti," amesema.
Kinachotia matumaini ni kwamba nchi nyingi za Afrika tayari zilikuwa zinachunguza abiria wanaowasili katika viwanja vyao vya ndege kwasababu ya ugonjwa wa Ebola.
Nchi ambazo zilikuwa zinakabiliana na Ebola bado zina vituo vilivyotengwa na wataalamu kama njia moja ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
Lakini linapokuja suala la kutambua, Ebola ni tofauti kabisa na virusi vya corona.
Ebola inaambukiza tu wakati dalili zimeanza kujitokeza lakini kuna taarifa kwamba katika baadhi ya visa, virusi vya corona huenda vikasambaa hata kabla mgonjwa kuanza kuonesha dalili zozote.
Jifunze zaidi kuhusu virusi vya vipya vya corona
- Virusi vya Corona vinasambaa kabla ya dalili kuanza kujitokeza
- Je tunafaa kuwa na wasiwasi kuhusu virusi vya Corona?
- Je ni ugonjwa gani huu unaosambaa kwa kasi China?
- Coronavirus: Je 'kuziba pua' kunaweza kuzuia maambukizi?
- Afrika Mashariki yachukua tahadhari dhidi ya maambukiza ya virusi vya Corona
Vipi kuhusu usafiri kati ya Afrika na Uchina?
Uhusiano wa karibu wa kibiashara kati ya Uchina na nchi za Afrika umezua wasiwasi kwamba huenda virusi hivyo vikasambaa.
Uchina ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Afrika na karibia makampuni 10,000 ua Uchina kwasasa yanaendesha shughuli zao kote barani humo. Chombo cha habari cha Uchina kimesema zaidi ya raia milioni moja wa uchina wanaishi Afrika.
Pia kuna zaidi ya wanafunzi 80,000 wa Afrika nchini Uchina, wengi wao wakiwa wameenda kusoma baada ya kupata ufadhili wa masomo gazeti la the Guardian limesema.
Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 21 kutoka Cameroon alisemekana kwamba amepata virusi hivyo baada ya kwenda mji wa Wuhan na kwasasa anaendelea kupata matibabu.
Wanafunzi wa Uchina pia wanasafiri kote barani Afrika vilevile kwasababu ya ufadhili za masomo.
Mashirika mengi ya ndege kote duniani yamesitisha safari zake za ndege kwenda Uchina. Vilevile, Mashirika ya ndege za Afrika yamekuwa na shinikizo kubwa la kusitisha safari zake.
Mashirika ya ndege ya Mirsi, Kenya, Morocco na Rwanda yamesitisha safari zake lakini shirika kubwa zaidi la ndege barani humo Ethiopia bado linaendelea na safari zake kama kawaida.
Shirika la WHO limeshauri dhidi ya kuweka vikwazo vya usafiri na badala yake limebaini nchi 13 Afrika, ambazo zimetakiwa kuwa na tahadhari ya hali ya juu kwasababu ya uhusiano wake wa moja kwa moja na Uchina. Pia linapanga kutoa usaidizi kwa nchi hizo 13 kufikia mwishoni mwa wiki hii.
Je nchi 13 zinazopewa kipaumbele na WHO barani Afrika ni zipi?
- Algeria
- Angola
- Democratic Republic of Congo
- Ethiopia
- Ghana
- Ivory Coast
- Kenya
- Mauritius
- Nigeria
- South Africa
- Tanzania
- Uganda
- Zambia