Ireland yafanya uchaguzi mkuu

Admin
By -
0
Raia wa Ireland wanapiga kura leo kumpata waziri mkuu mpya huku kukiwa na uwezekano wa chama cha Republican, Sinn Fein kinachoegemea siasa za mrengo wa kushoto kuvishinda vyama vikuu viwili kwa mara ya kwanza.
Wapiga kura wanateremka vituoni katika uchaguzi ambao hasira kutokana na sera za uchumi za kubana matumizi na kadhia ya ukosefu wa nyumba za kuishi vimechochea kuimarika kwa chama cha kizalendo kinachoegemea siasa za mrengo wa kushoto, Sinn Fein.
Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema asubuhi na matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa muda mfupi baada ya kufungwa vituo vya kupigia kura alasiri ya leo.
Matokeo ya mwisho ya maoni ya umma yanaonesha chama cha Sinn Fein kinachuana vikali na chama cha waziri mkuu Leo Varadkar cha Fine Gael na kile cha upinzani Fianna Fail, vyama viwili ambavyo vimetawala siasa za Ireland tangu uhuru wa taifa hilo.

Fenn Fein itaweza kuunda serikali?

Kuongezeka uungaji mkono kwa Sinn Fein ambacho kimesisitiza lengo lake la kuiunganisha tena Ireland, kunatishia uzani wa kisiasa nchini Ireland licha ya kwamba chama hicho hakitokuwa na uwezo wa kuunda serikali baada ya uchaguzi kwa sababu vyama vya Fine Gael na Fianna Fail vimekataa kushirikiana nacho.
Sinn Fein moja ya vyama vikubwa Ireland ya Kaskazini iliyo sehemu ya Uingereza lakini kwa muda mrefu kimekuwa chama chenye nafasi finyu nchini Ireland kutokana na kuandamwa na vyama vikuu kuhusiana na mahusiano yake na kundi la wapiganaji wa IRA wanaotaka kujitenga kwa Ireland Kaskazini kutoka Uingereza.
Hata hivyo mapendekezo ya chama hicho ya kutaka kushughulikia kadhia ya ukosefu wa makaazi na mfumo wa afya ya taifa nchini Ireland yamewavutia wapiga kura.
"Nadhani kuna ulazima wa kufanya mabadiliko " amesema Noleen Kelly anayefanya kazi na sekta ya umma katika moja ya vituo vya kupigia kura kwenye mji mkuu wa Ireland, Dublin.

Varadkar yaonya dhidi ya kukichagua chama cha Fenn Fein

Waziri Mkuu wa Ireland, Leo Varadkar

Kupitia ujumbe katika ukurasa wa Twitter hapo jana, waziri mkuu anayeondoka wa Ireland, Leo Varadkar ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Fine Gael amewaonya wapiga kura dhidi kukichagua chama cha Sinn Fein, akidai kilifanya uharibifu kilipokuwa madarakani.
Wakati wa mkutano wa mwisho wa chama cha Fine Gael na wanahabari siku ya Alhamisi, Varadkar alisema kukipigia kura chama cha Sinn Fein kutahatarisha kila kitu ikiwemo uchumi na taasisi za kidemokrasia nchini Ireland.
Vyama vikuu viwili Fine Gael na Fianna Fail ambavyo asili yake ni pande mbili zilizopingana wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ireland vya mwaka 1992, ni mahasimu wa jadi lakini vina mtizamo wa pamoja chini ya siasa za wastani zinazoegemea mrengo wa kulia.
Kwa miongo kadhaa vyama hivyo vimekuwa vikibadilishana hatamu za uongozi nchini Ireland.
Hata hivyo uungwaji mkono wa vyama hivyo viwili umeporomoka tangu mdodoro wa uchumi wa mwaka 2008 ulioathiri kwa sehemu kubwa uchumi wa Ireland na kuandamwa na madeni.
Ireland ilikaribia kufilisika hatua iliyoilazimisha kuomba msaada wa uokozi kutoka jumuiya ya kimataifa uliofuatiwa na miaka kadhaa ya sera za kubana matumizi.
Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)