Bunge la Wawakilishi nchini Marekani limepitisha azimio linalolenga kumzuia Rais Donald Trump kupigana vita na Iran. Bunge hilo ambalo linafahamika pia kama Kongresi limepitisha azimio hilo kwa kura 224 dhidi ya 194.Hata hivyo azimio hilo lililopitishwa na Kongresi ambayo ina wawakilishi wengi zaidi wa Democrats litakutana na wakati mgumu kwenye bunge la Seneti linalotawaliwa na wawakilishi wengi zaidi kutoka chama cha rais Trump cha Republicans.
Azimio hilo linalenga kuipa Kongresi nguvu ya kutoa kibali cha shambulio lolote dhidi ya Iran, isipokuwa pale tu patakapokuwa na shambulio la ghafla dhidi ya Marekani. Kwa sasa hakuna upande kati ya Iran na Marekani ambao umetamka kuwa utaendelea na mashambulizi. Jumatano wiki hii, Iran ilishambulia kambi mbili za kijeshi za Marekani nchini Iraq baada ya Marekani kumuua Jenerali wa Iran Qasem Soleimani wiki iliyopita.
Azimio linamtaka rais Trump "kuacha kulitumia jeshi la Marekani" dhidi ya Iran mpaka apate kibali cha Kongresi. Mwanya pekee unaopendekezwa wa kufanya shambulizi bila kibali ni pale itakapohitajika "kujilinda dhidi ya shambulio (kutoka Iran)."Hata kama azimio hilo litapita Seneti bado Trump hatalazimika kulipigia kura ya turufu kwa kuwa halimfungi mikono moja kwa moja. Msingi wa azimio hilo unatokana na sheria ya vita ya Marekani ya maaka 1873 ambayo inaipa nguvu Kongresi kukagua mamlaka ya rais kabla ya kupeleka majeshi vitani. Hata hivyo maswali ya kisheria iwapo aina hiyo ya azimio inaweza kumbana rais bado hayajapatiwa ufumbuzi.
Spika wa Kongresi Bi Nancy Pelosi ambaye anatokea chama cha Democrats amesema kuwa haamini kama Trump ameifanya Marekani kuwa salama kwa kumuua Jenerali Soleimani. Kiongozi wa Republican ndani ya Kongresi Kevin McCarthy ameliita azimio hilo kuwa halina maana huku mnadhimu wa chama hicho akilinanga kuwa ni "taarifa kwa vyombo vya habari".Trump, kupitia ukurasa wake wa Twitter aliwaasa wawikilishi wote wa Republican "wapige kura ya kulikataa azimio hilo la wazimu la Pelosi." Pia ametoa shutuma mpya zinazodai kuwa taarifa za kijasusi zinaonesha kuwa Iran inapanga kushambulia ubalozi wa Marekani Baghdad, Iraq kwa makombora.