NYOTA wa miondoko ya R&B, R Kelly, ameonyesha masikitiko yake katika kipindi kimoja cha asubuhi cha televisheni dhidi ya tuhuma za unyanyasaji wa kingono zinazomkabili .
Ikiwa ni mara ya kwanza mwanamuziki huyo kuhojiwa tangu akamatwe na polisi mwezi uliopita alisema,”Sijafanya vitu hivyo, huyo si mimi” na kusisitiza kuwa anapambania maisha yake.
Mwendesha mashitaka wa Chicago alimfungulia Kelly mashtaka 10 yanayohusiana na makosa ya unyanyasaji wa kingono, huku yakihusisha waathirika wanne ambao watatu kati yao walifanyiwa unyanyasaji wakiwa na umri chini ya miaka 18.
Mwanamuziki huyo alisisitiza kutokuwa na hatia kwa mashtaka yote yanayomkabili na sasa yuko nje ya gereza kwa dhamana. Kama atapatikana na hatia, mwanamuziki huyo atafungwa kati ya miaka mitatu hadi sita kwa kila kosa.
Mwaka 2002, Kelly alikabibiliwa na mashitaka 21 ya kutengeneza filamu ya ngono na msichana ambaye alidaiwa kuwa chini ya umri wa miaka 18.
Na hatimaye jaji alihitimisha kesi hiyo kwa kusema kuwa hawawezi kuthibitisha umri wa binti yule kupitia mkanda wa video na hivyo kumpelekea Kelly kupatikana hana hatia kwa mashitaka yote 21.
Mwanamuziki huyo akizungumza na mwandishi Gayle King, Kelly alisema kesi ile ya awali imetumika dhidi ya mashitaka haya mapya ili kuaminika kuwa ana makosa kweli.
“Wanaangalia makosa ya nyuma na wanajaribu kuyaongeza katika madai ya sasa ili nionekane kuwa ninahusika, hicho ndicho kinachoendelea” Kelly alisema.
“Lakini mambo hayo ya nyuma yanahusiana na vitendo vya ngono vya wasichana wadogo pia?” mwandishi alimuuliza.
“Si kweli kabisa, hayana uhusiano wowote,” Kelly alinyanyuka na kupinga kwa msisitizo na kuongeza kuwa hawawezi kuendelea kumhukumu kwa kesi ambayo alishinda na alikutwa hana hatia.
Mwanamuziki huyo alikana kuhusika na shutuma ambazo zilitolewa hivi karibuni dhidi ya makala yake mpya ya ‘Surviving R Kelly’, ambapo alikuwa amewakamata wanawake bila idhini yao na kuchukua simu zao, kuwakataza kula na kuwazuia kuwasiliana na familia zao.
Kelly kwa hisia kali , alimuuliza mwandishi: “Inawezekana vipi mimi kuwa mpumbavu kiasi hicho, kwa kila kitu ambacho nimepitia katika maisha yangu, ninawezaje kumficha mtu? Ninawezaje kuwa mpumbavu kufanya kitu kama hicho? Tumia tu akili yako,”aliendelea kupaza sauti.
“Sahau kuhusu majarida, sahau namna ambavyo unajisikia juu yangu. Nichukie kama unataka, nipende kama unataka lakini tumia tu akili yako kunihukumu kwa kosa hili.
“Ninawezaje kuwa mpumbavu kiasi hicho kufanya jambo kama hilo sasa, ikiwa nina tuhuma nyingi ambazo nilizipitia miaka ya nyuma, kweli kabisa mimi nifanye makosa hayo sasa?”
“Nadhani lazima niwe mtu wa ajabu sana kufanya jambo kama hilo la kuwafungia wasichana bila idhini yao katika makazi yangu!” alizungumka huku analia na kusisitiza ,”Huyo si mimi!”
Kelly alikiri kufanya mambo mengi mabaya miaka ya nyuma lakini aliomba radhi kwa wanawake ambao alikuwa na mahusiano nao.
Kelly anaamini kuwa ni rahisi sana kwa msanii kushutumiwa na madai mbalimbali, kitu ambacho watu wanafanya ni kupiga simu tu. Anasema kupitia madai ya unyanyasaji wa ngono yanayomkabili hayana uhusiano kabisa na tabia zake
“Ninahitaji msaada, Ninahitaji mtu mwenye moyo wa kunisaidia anisaidie maana nina moyo mzuri lakini ninasalitiwa kila mara na ninaendelea kuwasamehe,” alisisitiza.
Mtangazaji mwingine alisema kuwa inawezekana ni kweli Kelly anahitaji msaada maana amekuwa anajibu kwa hisia kali mara nyingi.
Mtangazaji huyo aliwahoji pia wanawake ambao walikuwa wana uhusiano na Kelly hivi karibuni, Azriel Clary na Joycelyn Savage
“Ninalia kwa sababu nyinyi hamjui ukweli, huo wote ni uongo kwa sababu ya fedha na kama hamuoni hilo basi nyinyi ni wapumbavu!”
Wazazi wa Clay ambao wanadai kuwa Kelly anamshikilia binti yao bila idhini yake wanasema, ” Tunampenda sana binti yetu Azriel na tunamkumbuka sana,” alisema Alice na Angelo Clary.
“Azriel anasumbuliwa na afya ya akili kutokana na unyanyasaji aliofanyiwa na R Kelly, R Kelly ni muongo na lazima haki itendeke sasa kwa makosa yote ya unyanyasaji wa ngono yanayomkabili dhidi ya wasichana wadogo. Waathirika wote hawa na wazazi hawawezi kuwa wanadanganya.”