RAIS MAGUFULI AMTWISHA MPANGO ZIGO LA TTCL NA AIRTEL


Image result for picha ya jengo la airtel tanzaniaImage result for PIC YA WAZIRI MPANGOAIS John Magufuli amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango kufuatilia Kampuni ya Simu ya Mkononi ya Airtel ili kujua ukweli ili umiliki wake urudi serikalini kabla ya kuisha kwa mwaka huu.
Alisema hayo jana katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inayojengwa katika eneo la Makulu mjini hapa. 
Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Fedha na Mipango kufuatilia suala hilo haraka ili Airtel irudishwe kumilikiwa na serikali. “Fuatilia suala la Airtel, Airtel kwa taarifa tulizonazo ni mali ya TTCL (Kampuni ya Simu Tanzania).
Palifanyika mchezo wa hovyo, sasa sitaki kuzungumza mengi fuatilia. “Nchi hii ilikuwa ya maajabu sana unachukua share (hisa) leo, kesho inauzwa, kisha zinafutwa na kuuzwa juu kwa dola moja,” alisema Rais Magufuli.
 Taarifa kuhusu Airtel Taarifa za kuaminika kutoka serikalini, zinaeleza kuwa TTCL itamiliki hisa zote za Airtel Tanzania Limited, ambapo tayari TTCL imewasilisha hoja ya kutaka kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba serikali ilipunjwa kwenye hesabu za uwekezaji.
Inaelezwa kuwa hoja ya Airtel kuwa mali ya TTCL inaanzia Novemba 3, 1998, ilipoanzisha kampuni tanzu ya Cellnet ambayo ilifanya kazi mpaka Mei 7, 2001 ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel Tanzania, huku umiliki wake ukiendelea kuwa chini ya shirika hilo kwa asilimia zote baada ya kuwekeza dola milioni tano za Marekani (zaidi ya Shbilioni 11). Inaelezwa kuwa Januari 31, 2002, Celtel ikiwa chini ya umiliki wa TTCL ilikopa dola 82 milioni (zaidi ya Sh bilioni 180.4) ili kukuza mtaji wake.
Kwa kipindi hicho, TTCL iliyokuwa na thamani ya dola 600 milioni (zaidi ya Sh trilioni 1.32) ilikuwa inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi. Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 65 ya hisa zote na mbia huyo asilimia 35 zilizosalia.
 Agosti 5, 2005, mabadiliko yalifanywa kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa Celtel kwa lengo la kuunda kampuni mbili tofauti; Celtel ikatenganishwa na TTCL.
Kutokana na mabadiliko hayo, Celtel iliwekwa chini ya umiliki wa MSI ambayo Septemba 2007 iliuza hisa zake kwa Zain, ambayo nayo ilikuja kuziuza kwa Bharti Airtel Juni 8, 2010. Imeelezwa kuwa TTCL inadai uwekezaji wake ilioufanya Celtel baadaye Airtel, ambayo thamani yake imeongezeka maradufu sasa, haulingani na inachokipata, hivyo kutaka kusimamia biashara za kampuni hiyo ya mawasiliano.
Hoja ya madai hayo ni namna umiliki wa hisa ulivyobadilishwa baada ya Celtel kutenganishwa na TTCL, ambayo ilipewa hisa chache, tofauti na ilivyostahili. Kwa sasa, Airtel Tanzania inamilikiwa na Serikali yenye asilimia 40 na Celtel Tanzania BV, kampuni tanzu ya Zain Africa BV ambayo ilinunuliwa na Bharti Airtel International, Novemba, 2010 ikiwa na asilimia 60.
Katika mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni, Serikali iliilipa Bharti Airtel Sh bilioni 14.7 hivyo kuchukua asilimia 35 ya hisa ilizokuwa inamiliki na kuifanya imiliki asilimia zote za TTCL. Sheria mpya iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge, imeibadili TTCL inayohudumia asilimia 0.82 ya soko kuwa shirika la umma la mawasiliano na kulipa jukumu kubwa katika sekta ya mawasiliano nchini.
Bharti Airtel inatakiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kukidhi vigezo vya Sheria ya Posta na Mawasiliano ya mwaka 2010, lakini haijafanya hivyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post