AHADI ZA MO BAADA YA KUKABIZIWA TIMU YA SIMBA

Mfanya biashara maarufu nchini Mohammed Dewji MO ameshinda zabuni ya kuwekeza katika klabu ya Simba kwa ofa ya bilioni 20 za kitanzania.

MO ametangazwa mshindi wa dili hilo na Mwenyekiti wa kamati (Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu Thomas Mihayo) iliyokuwa ikisimamia mchakato mzima wa kumpata mwekezaji atakayekidhi vigezo na masharti.

Baada ya kutangazwa mshindi wa zabuni ya uwekezaji ndani ya Simba, MO ametoa ahadi kadha wa kadha ikiwemo kujenga viwanja viwili na kufanya usajili wa Tsh. 1 billion.

“Katika mwaka wa kwanza, nawaahidi kushirikiana nanyi tutakuwa na kiwanja cha nyasi asilia na kiwanja cha nyasi za bandia ambapo viwanja hivi tutavitumia kwa kadiri ya mahitaji ya mechi tutakazokwenda kucheza.”

“Tutajenga hostel ambayo itakuwa na vyumba 35 ambavyo wataishi wachezaji 30 pamoja na support staffs. Kila chumba kitakuwa na ukubwa wa square meter 35 kila unit itakuwa na chumba cha kulala, sebule, bafu na choo, samani za ndani AC, jiko na vitu vingine ili kufanya eneo hilo kuwa bora kwa wachezaji wetu”.

“Tumetenga pesa kwa ajili ya kujenga mgahawa ambao wachezaji watakuwa wanakula hapo, kutakuwa na gym ili wachezaji wetu wafanye mazoezi na kuwa na nguvu hii haitakuwa kama gym za kawaida kwa watu ambao wanajenga miili mikubwa au kupunguza uzito. Gym hii itakuwa na vifaa maalum kwa ajili ya kuimarisha misuli kwa wachezaji wetu.”

“Tutajenga vyumba ambavyo vitatumika kuwanfanya wachezaji recovering, kutakuwa na swimming pool, lakini pia kama wachezaji wanataka kuburudika, kutakuwa na sehemu ya play station,  table tenis na mambo mengine ya kuwaburudisha.”

“Ili kuwa na wachezaji bora kwa miaka ijayo tunahitaji kuwa na kituo cha kukuzia vipaji kwa watoto chini ya miaka 14, 16, 18, mipango yetu ya baadaye ni kushirikiana na timu kubwa za Ulaya kutuongoza na kutuelimisha ni jinsi gani ya kujenga kituo chenye hadhi ya kimataifa na Mungu akipenda tutakuwa na kituo bora barani Afrika.”

“Wote tunaopenda mpira tunajua kama ukitaka kuwa na wachezaji bora lazima utumie pesa, nia yetu kwa mwaka wa kwanza tunatarajia pesa usajili kiwango cha chini iwe bilioni moja. Pia tumetenga zaidi ya milioni 500 kuboresha benchi la ufundi kwa kushirikiana na benchi lililopo sasa.”

“Tutakuwa na chumba maalum cha mawasiliano ambapo kwa sasa tuna Simba TV ambayo haina taarifa za kutosha kuhusu klabu. Tunategemea Azam TV kututengenezea vipindi lakini sasa tutakuwa na vifaa vyetu wenyewe ili tuweze kufanya uchambuzi bora na wa kisasa kuhusu mwenendo wa timu yeu. Katika hicho chumba kitakuwa na uwezo wa kurekodi kila mchezo wa Simba kila mazoezi ya Simba ili kuweza kuelimisha wachezaji jinsi gani ya kuboresha viwango vyao mmojammoja na kama timu.”

“Tuna mambo mengi sana ya kuifanyia klabu yetu, ninaloamini sasa Simba itakuwa klabu tajiri kupita zote katika ukanda wa huu wa Afrika Mashariki na Kati, utajiri huu utaenda pamoja na kutengeneza brand ya Simba.”

“Shabaha ya Simba si kushindana tena na timu za nyumbani pekee, sasa lazima tukashindane na TP Mazembe, Zamalek Eparance na vilabu vingine vikubwa vya Afrika. Ukubwa wetu sisi usiishie kugombea ubingwa wa Tanzania tu, lazima tukapiganie mataji ya Afrika ambayo ndio heshima inayostahili nchi yetu ya Tanzania pamoja na timu yetu ya Simba. Ili kufanikisha hilo lazima tununue wachezaji bora watakaowezesha kufikia malengo hayo.”


Post a Comment

Previous Post Next Post