DIWANI WA CHADEMA ALIYE REKODI AKIPEWA RUSHWA AJITOKEZA


Arusha. Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, wamewahoji kwa zaidi ya saa sita, madiwani waliojiuzulu Chadema wanaotuhumiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kuwa walipewa rushwa.

Waliofika Takukuru ni Catherine Mtui, aliyekuwa diwani wa viti maalumu, Japhet Jackson (aliyekuwa diwani wa Ambuleni) na Bryson Isangya (aliyekuwa diwani wa Maroroni). Baada ya kuhojiwa hawakutaka kuzungumza chochote wakisema wanaacha uchunguzi uendelee.

Pamoja nao, diwani wa Mbuguni, Ahimidiwe Rico anayedaiwa kuwa ndiye alirekodi sauti na picha wakati akishawishiwa na viongozi wa Serikali na wa Halmashauri ya Meru amehojiwa kwa zaidi ya saa tatu leo Jumanne Oktoba 17, 2017.

Rico amesema amewaeleza Takukuru kila kitu ambacho anakifahamu katika sakata hilo, ikiwemo kuwarekodi viongozi ambao walimshawishi kujiuzuru udiwani.

"Msimamo wangu ni kwamba, nachukia rushwa. Nimewaeleza kila kitu na wao waliniuliza kuhusu vifaa nilivyotumia kuwarekodi nikawaambia ni mali ya mbunge, alivitoa nchini Uingereza," amesema.

Rico aliyesindikizwa na diwani wa  Nkwanankore, Wilson Nanyaro amesema  ana imani na Takukuru kwamba watafanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua.



Post a Comment

Previous Post Next Post