WABUNGE WA CUF WAMVAA SPIKA WA BUNGE
By -
November 27, 2017
0
Dar es Salaam. Wabunge wanane wa viti maalumu CUF waliovuliwa ubunge wamemwandika barua Katibu wa Bunge amjulishe Spika Job Ndugai kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu ili achukue hatua stahiki ikiwamo kuwafahamisha utaratibu utakaotumika kuwarejesha kwenye nafasi zao.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika uamuzi iliyoutoa Novemba 10, imeizuia CUF kujadili na kuwafukuza uanachama wabunge hao na madiwani wawili wa viti maalumu.
Wakati Mahakama ikitoa uamuzi huo, tayari chama hicho kikiwa kinachoongozwa na mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kilishawavua uanachama hivyo kupoteza ubunge wao.
Wabunge hao wanaomuunga mkono katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ni Miza Bakari Haji, Saverina Mwijage, Salma Mwasa, Raisa Mussa, Riziki Mngwali, Hadija Salum Al-Qassmy, Saumu Sakala na Halima Mohamed.
Hatima yao
Akizungumza jana kwa niaba ya wenzake, Mngwali alisema waliandika barua Novemba 20 na tayari imepokewa katika ofisi ya Bunge.
“Kisheria sisi bado ni wanachama halali wa CUF tuna sifa za kuendelea kuwa wabunge kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu, ndiyo maana tumemwandikia Spika ili kujua utaratibu utakaotumika kuturejesha bungeni kwa spidi ileile iliyotumika kutuengua katika chombo hicho Julai 25,” alisema.
Mngwali aliyeambatana na Mwasa na Mwijage, alisema wameona ni vyema kuwajulisha wanachama wa CUF na Watanzania hatua walizochukua baada ya uamuzi wa Mahakama.
Alisema wana imani Spika Ndugai atatenda haki katika jambo hilo. Julai 25, Spika Ndugai aliridhia barua ya Profesa Lipumba ya kuwavua uanachama wabunge hao.
Baadaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ilitangaza wabunge wapya baada ya kupata taarifa ya Bunge.
Wabunge walioteuliwa kuchukua nafasi zao ni Sonia Magogo, Kiza Mayeye, Shamsia Mtamba, Zainab Mndolwa, Hindu Mwenda, Alfredina Kahigi, Nuru Bafadhili na Rukia Ahmed Kassim.
Kabla ya kuapishwa, Hindu alifariki dunia Septemba mosi na NEC ilimteua Rehema Migira kuchukua nafasi yake.
Kaimu naibu mkurugenzi wa habari, mawasiliano kwa umma wa CUF, Mbarala Maharagande alisema uamuzi wa Mahakama umeshatoka hivyo wanasubiri busara za Ndugai za kuwarejesha wabunge hao.
Hata hivyo, Ndugai alipotafutwa kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari kujibu lolote
Tags: