KLABU ya Yanga imeingia mkataba wa miezi sita na Shirika la Umoja wa Mataifa la Unicef kwa ajili ya kutoa elimu na kuwapa taarifa Watanzania kuhusu Corona na namna ya kujikinga na kuchukua tahadhari kuhusu Ebola.
Injinia Hersi Said Rais wa Yanga amesema kuwa ni furaha kubwa kwa ajili ya timu hiyo kuingia makubaliano na Shirika la Umoja wa Mataifa.
“Kutokana na kuwa karibu na jamii kwa kurejesha kwa jamii hilo limewashawishi Unicef kufanya kazi na sisi kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa jamii.
“Sisi kazi yetu ya mpira tunafanya kazi na mashabiki kwa kuwapa burudani hivyo wakiwa na afya inakuwa ni rahisi kwetu kuendelea kuwapa burudani jambo ambalo tunalifanya kwa sasa.
“Tunaunga mkono juhudi za Serikali kwenye kupambana na Corona pamoja na kutoa elimu kuhusunamna ya kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya Ebola,” amesema.
Fatimata Balandi mwakilishi kutoka Unicef amesema kuwa wanafurahi kufanya kazi na Yanga kwa ajili ya kufikisha elimu kwa jamii.