
Hawezi kusaini mfungwa yeyote aliyehukumiwa adhabu hiyo kwenda kunyongwa.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, baada ya mahakama kumtia mtu hatiani na kumsomea adhabu ya kunyongwa mpaka kifo, mamlaka ya kutekelezwa kwa adhabu hiyo inabidi kwanza yapate ridhaa ya kiongozi mkuu wa nchi, tena kwa kutia saini.
Mara ya mwisho kwa mfungwa kunyongwa ilikuwa mwaka 1994, enzi za utawala wa Rais wa awamu ya pili wa nchi hiyo, Ally Hassan Mwinyi.
Baada ya Mwinyi akaja rais Benjamin Mkapa ambaye akamwachia kijiti Jakaya Mrisho Kikwete na wote hao hawakusaini mfungwa yeyote kunyongwa.
Mwaka 2017, Magufuli akiwa anamuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamisi Juma alivunja ukimya juu ya suala hilo
"Sisi wanasiasa tunaogopa kunyonga, natambua kwa sasa orodha ya watu ambao wanatakiwa kunyongwa ni kubwa sana, ila mimi naomba hiyo orodha msiniletee kwa sababu najua ugumu wake ulivyo," alisistiza.
Lakini licha ya marais walopita kutokuidhinisha kutekelezwa kwa adhabu hiyo pamoja na Magufuli kuendeleza msimamo huo, bado adhabu hiyo ipo kisheria.
Kutokana na hilo, wanaharakati kutoka kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na mawakili kadhaa walifungua shauri la kutaka adhabu hiyo ifutwe kisheria.
Leo hii Mahakama Kuu ya nchi hiyo inatarajiwa kutoa hukumu juu ya shauri hilo.

Mpaka sasa mahakama za Tanzania zinaendelea kutoa adhabu hiyo kwa wale ambao wanakutwa na hatia kwa mashtaka stahiki.
Matokeo yake idadi ya wafungwa wanaosubiri kunyongwa magerezani inaongezeka, na inakisiwa wanazidi 400.
Wanaharakati wanaipinga vikali adhabu hiyo, na kudai kuwa inakiuka haki ya msingi ya kuishi.
Pia kwa nchini Tanzania, wanaharakati hao wanadai wafungwa wanaosubiri kunyongwa wanapitia changamoto kubwa za msongo wa mawazo kwani hawajui lini adhabu hiyo itatekelezwa na baadhi wanasubiri kwa zaidi ya miongo miwili sasa.
Hukumu ya kifo duniani
Harakati za kupinga hukumu ya kifo duniani zimepamba moto.
Kwa mujibu wa shirika la kmataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International mpaka kufikia 2017 nchi 142 zimeacha kutoa hukumu ya kifo kisheria na/au kiutekelezaji.
Umoja wa Mataifa (UN) unakadiria kuwa nchi 170 zimeachana na adhabu hiyo kwa nman moja au nyengine.
UN ina wanachama 193, hivyo ni mataifa 23 tu ndio ambayo inawezekana walitoa hata hukumu moja ya kifo katika muongo uliopita.

Mataifa ambayo yametekeleza hukumu ya kifo kati ya mwaka 2013 na 2017
Afghanistan, Bahrain, Bangladesh, Belarus, Botswana, Chad, China, Egypt, Equatorial Guinea, India, Indonesia, Iran, Iraq, Japan, Jordan, Kuwait, Malaysia, Nigeria, Korea Kaskazini, Oman, Pakistan, Palestina,
Saudi Arabia, Singapore, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Taiwan, Thailand, United Arab Emirates, Marekani, Vietnam na Yemen.
Nchi ambazo hazijatekeleza adhabu hiyo licha kuwepo kisheria kati ya 2013 na 2017
Tanzania si nchi pekee ambayo haitekelezi adhabu hiyo licha ya kuwepo kisheria.
Nchi nyengine zinazofanya hivyo ni pamoja na Antigua na Barbuda, Bahamas, Barbados, Belize, Comoros, Cuba, Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Dominica, Ethiopia, Gambia, Guyana, Jamaica, Lebanon, Lesotho, Qatar, Saint Kitts na Nevis, Saint Lucia, Saint Vincent na Grenadines, Trinidad na Tobago, Uganda na Zimbabwe.