Katibu mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais ,Mhandisi Joseph Malongo ametangaza operesheni maalum ya Nchi nzima ya uzingatiaji wa Sheria ya usimamizi wa Mazingira juu ya marufuku ya Mifuko ya Plastiki na Matumizi endelevu ya mifuko mbadala .
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma Mhandisi Malongo amesema kanuni za usimamizi wa Mazingira za kupiga marufuku mifuko ya Plastiki za mwaka 2019 zimeanza kutekelezwa kuanzia tarehe Mosi ,Juni,2019 hivyo kwa mujibu wa kanuni hizo ,ni marufuku kuzalisha,kusambaza kuingiza nchini ama kusambaza nje ya nchi na kutumia Mifuko ya Plastiki iliyotajwa katika katazo hilo .
Mhandisi Malongo amebainisha ,kiwanda,kikundi cha watu au mtu binafsi atakayebainika kukiukwa matakwa ya kanuni hizo atakuwa ametenda kosa la jinai na hivyo sheria itachukua mkondo wake.
Hata hivyo,amesema baada ya kuanza kwa utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki,baadhi ya wazalishaji na wasambazaji wamebadilisha matumizi ya mifuko laini ya plastiki isiyokuwa na mishikio na kuitumia kama vibebeo vya bidhaa kinyume na kanuni ya 8 ya kanuni za usimamizi wa Mazingira.
Mhandisi Malongo ameendelea kufafanua kuwa kanuni ya 9 inatoa Msamaha kwa baadhi ya vifungashio vya plastiki kwa ajili ya huduma za afya au kwa vifungashio vinavyotumika kufungashia bidhaa za viwandani ,sekta za ujenzi ,sekta ya kilimo,vyakula au usafi na udhibiti wa taka.
Shirika la viwango Tanzanzia TBS linaandaa viwango vya vifungashio ambavyo vitalazimisha kiwango cha unene,uwekwaji lakiri na kutambulisha bidhaa iliyofungashwa kabla ya kuuzwa.
Katika kuhakikisha suala hilo linatekelezwa kwa ufanisi zaidi,Mhandisi Malongo amesema Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini,[NEMC] linaendelea na Operesheni kabambe nchi nzima ya kusaka mifuko ambayo imebadilishiwa matumizi yake na kukiuka sheria ambapo operesheni hiyo itahusisha vyombo vya ulinzi na usalama,kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya,mamlaka za serikali za mitaa.
Vingine ni mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali,shirika la viwango Tanzania TBS,Mamlaka ya Chakula na Dawa ,TFDA,Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,Pamoja na mamlaka ya viwanja vya ndege,bandari ,Forodha,uhamiaji na usafiri wan chi kavu.
Ikumbukwe kuwa ni makosa kisheria kubadili matumizi ya vifungashio na kuwa mifuko ya kubebea bidhaa na adhabu stahiki zitatolewa kwa watu watakaobadili matumizi ya vifungashio na kuwa vibebeo vya bidhaa huku Ofisi ya Makamu wa Rais ikiendelea kuelimisha umma pia ikisisitiza kutumia mifuko mbadala.