Rais wa Zimbabwe Robert Mgabe |
Rais wa Zimbabwe Robert Gabriel Mgabe amekataa kuondoka madarakani na kusisitiza kuwa yeye ndiye kiongozi halali wa Zimbabwe na hataki kushiriki mazungumzo yanayofanywa na Kasisi mmoja wa Kikatoliki ya kumuezesha rais huyo mwenye umri wa miaka 93 kuondoka madarakani kwa amani baada ya mapinduzi ya kijeshi.
Duru ya kisiasa ambayo ilizungumza na washirika wa ngazi ya juu waliowekwa katika kizuizi cha nyumbani pamoja na mkewe, Grace, nyumbani kwa kiongozi huyo mjini Harare, zimesema kuwa Mugabe hana mipango ya kujiuzulu kwa hiari kabla ya uchaguzi unaopangwa mwaka ujao.
Upinzani nchini humo umemtaka Mugabe ajiuzulu mara moja na kuundwa haraka serikali ya mpito.
Katibu Mkuu wa chama cha MDC-T chake Morgan Tsvangirai amesema wanaunga mkono hatua ya jeshi lakini nchi inapaswa kurejeshwa haraka katika uongozi wa kikatiba.
Wajumbe maalumu waliotumwa na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma wanafanya mazungumzo kuhusu hatima ya Mugabe na viongozi wa Zimbabwe.
Nao maafisa kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika - SADC wanakutana baadaye leo katika mji mkuu wa Botswana, Gaberone kuijadili hali hiyo,
katika Mazungumzo hayo Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa Balozi Augustine Mahiga.
Wakati huo huoRais wa Umoja wa Afrika Alpha Conde amesema umoja huo hautaruhusu mapinduzi ya kijeshi nchini Zimbabwe.
Katika mahojiano na wanahabari mjini Paris, Ufaransa Rais Conde ambaye ni Rais wa taifa la Guinea ametaka kuheshimiwa kwa katiba na kurejea kwa utawala unaotambulika kikatiba akiongeza kuwa wanafahamu yanayojiri Zimbabwe ni matatizo ya ndani ambayo yanahitaji kusuluhishwa kisiasa na chama tawala cha ZANU PF na sio kwa kuingiliwa na jeshi.
Naye Makamu wa rais wa zamani wa Zimbabwe Joice Mujuru anasema ipo haja ya kufanyika mazungumzo ya serikali ya mpito ambayo itashughulikia masuala muhimu ya kuufufua uchumi na michakato ya uchaguzi.
Hali ya utulivu inaendelea kushuhudiwa nchini humo huku wanajeshi wakiendela kushika doria katika mji mkuu Harare.