Header Ads Widget

SIMBA YAFUNGUKA KUHUSU KOCHA WAO MPYA


 AHMED Ally ambaye ni Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, amefurahishwa na mabadiliko ya muda mfupi ya kikosi chao ikiwa ni siku chache tangu Kocha Mkuu raia wa Algeria, Abdehak Benchikha akabidhiwe timu.

Kocha huyo mara baada ya kutangazwa kuinoa timu hiyo, aliahidi makubwa msimu huu ikiwemo kuipa makombe yote wanayoshindania sambamba na burudani ya soka safi.

Akizungumza na Spoti Xtra, Ally alisema kuwa kocha wao Benchikha anastahili pongezi nyingi, ni baada ya kukifanyia mabadiliko kikosi, ambacho ndani ya siku chache fitinesi za wachezaji imeongezeka.

Ally alisema kuwa ufundi, hali ya kujiamini na morali imeongezeka, hiyo itawafanya wachezaji wao wapambane katika michezo yao inayofuatia ligi na michuano ya kimataifa.

Aliongeza kuwa, anataka kuona kiwango hicho cha kila mchezaji kikiendelea kuongezeka, ili kufikia malengo ya msimu huu kuwapoka Yanga mataji waliyoyachukua katika misimu miwili ligi na Kombe la FA.

“Benchikha amethibitisha ubora wake ndani ya siku chache ambazo, tumemkabidhi jukumu la kuifundisha timu yetu, amefanikiwa kufanya mabadiliko makubwa katika timu.

“Simba iliyocheza mchezo dhidi ya Wydad Casablanca, ndiyo Simba tunayoijua sisi inapiga pasi na kutawala mchezo, licha ya matokeo mabaya tuliyoyapata ya kufungwa bao 1-0.

“Ninasubiria Simba bora na imara itakayobeba mataji yote ya ndani na kufika mbali kimataifa, chini ya kocha mwenye CV kubwa Afrika,” alisema Ally.

Post a Comment

0 Comments