Kondakta wa Basi la Kampuni ya ABC aliyetambuliwa kwa jina moja la Pendo, amefariki dunia, huku watu 12 wakijeruhiwa baada ya basi hilo kuligonga lori lililokuwa limeegeshwa eneo la Chinangali mkoani hapa.
Majeruhi wa basi hilo wamesema ajali hiyo ilitokea jana saa 4.00 usiku wakiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Dodoma.
Akizungumza leo Jumatano Desemba 13, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, mkazi wa Nkhungu mkoani hapa, Theodata Bali amesema ametokea Zanzibar yeye na mjukuu wake ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, Baraka Waldi.
Amesema waliondoka saa 7.30 mchana jijini Dar es Salaam na mwendo wa dereva wa basi hilo hakuwa mzuri tangu walipoanza safari.
“Tulinusurika kupata ajali mkoani Morogoro ilikuwa alivae Semi trailer upande wake. Bahati lile semi treiler lilikuwa na breki nzuri kwa hiyo lilifunga breki na yeye (basi) akafunga breki na kuzimika papo hapo,” amesema.
Amesema yeye hupanda mabasi hayo mara nyingi lakini kwa siku ya jana alishangaa mwendo wa basi hilo, lakini waliponusurika kwa mara ya kwanza akajua atajirekebisha.
Hata hivyo, amesema hali ilibadilika kwa muda lakini lilipoanza kuingia giza alianza tena kuongeza mwendo na walipofika Chinangali ndipo walipata ajali, baada ya basi hilo kuligonga lori kwa nyuma. “Nilikuwa nimeanza kusinzia nilipostuka nikakuta mbele ya basi kote kuko wazi. Mimi nilikuwa nimekaa nyuma ya kiti cha kondakta nilirukiwa na vioo, ndio maana macho yamekuwa mekundu, mbele yetu alikuwa amekaa kondakta (aliyefariki), alikuwa amebanwa sana,” amesema.
Amesema alikuwa amebanwa miguu hivyo walivutia kiti ndipo akaitoa. “Dereva wa basi alitimua mbio baada ya kusababisha ajali,”amesema. Amesema yeye amepata jeraha mkononi, uso na machoni kutokana na vioo vilivyomruhia, huku mjukuu wake akijeruhiwa katika kidevu ambapo amefanyiwa upasuaji leo asubuhi.