Watu 33 wafariki baada ya jengo kuporomoka nchini Cameroon

Admin
By -
0


 Watu 33 wamefariki katika jiji kubwa la Cameroon baada ya jengo la ghorofa nne kuporomoka na kuangukia kwenye jengo jingine la makazi, wazima moto wamesema.

Tukio hili limetokea mapema Jumapili asubuhi katika mtaa wa Ange Raphaël wa Douala lakini sababu ya ajli hiyo bado haijafahamika.

Takriban watu 21 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa wanapokea matibabu katika hospitali ya karibu ya Laquintinie.

Msichana wa miaka mitatu ambaye alipelekwa hospitalini siku ya Jumapili alifariki baadaye.

Majirani waliofadhaika wamekuwa wakitafuta manusura kwenye vifusi pamoja na huduma za dharura.

Gavana wa mkoa, Samuel Dieudonné Ivaha Diboua, ametaka kuwatuliza watu - akisema hali imedhibitiwa na timu za uokoaji zitahakikisha hakuna mtu anayeachwa chini ya mabaki.

Afisa wa ngazi ya juu ameiambia BBC kuwa amesikitishwa sana kwamba maisha ya watu yamepotea licha ya hatua zilizopigwa katika miaka ya hivi karibuni kuimarisha usalama.

"Tumekuwa na furaha kutokumbwa na majanga kama hayo kwa muda sasa - hasa huko Douala ambako meya anajaribu kuleta utulivu," anasema Kizito Ngoa, mkuu wa Agizo la Wahandisi wa Ujenzi la Cameroon ambalo linadhibiti makazi nchini humo.

Tangu jengo kubwa la mwisho la Douala kuporomoka mwaka wa 2016, halmashauri ya jiji imekuwa ikizibomoa nyumba zinazoonekana kuwa hatarini kutokana na mafuriko au maporomoko ya ardhi, lakini jengo la ghorofa nne lililoporomoka siku ya Jumapili halikutengwa kwa ajili ya kubomolewa.

Wakazi waliambia wanahabari ilionekana kuwa mbovu lakini maafisa wa eneo hilo hawajathibitisha kilichosababisha ajali hiyo.

Katika taarifa ya Jumapili walimkumbusha yeyote anayetaka kujenga nyumba huko Douala kwamba lazima kwanza apate kibali rasmi na kisha na "kujenga tu muundo ulioidhinishwa".

Bw Ngoa anaambia BBC kwamba kushindwa kufuata sheria zilizowekwa ni mojawapo ya sababu kuu za kuporomoka kwa majengo kote nchini, na anasema gharama halisi ya mradi wa ujenzi inapaswa kuwekwa wazi kwa umma.

"Kuna hisia iliyoenea kwamba kila mtu anaweza tu kufanya kile anachotaka" na "ni wazi kuna hamu hii ya kuokoa pesa katika hatua zote za mradi".

Wakati mwingine wafanyakazi wa baraza wanashiriki katika hili, anasema, na vikwazo na maswali yanapotokea hayatangazwi vya kutosha.

Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)