Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya umesitisha maandamano ya kuipinga serikali yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kote nchini Jumatano wiki hii.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni, muungano huo ulisema badala ya kuingia mitaani, watafanya "gwaride za mshikamano na mkesha kwa wahasiriwa wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali katika maeneo yote ya nchi."
Muungano huo umewahimiza wafuasi wake kujitokeza na kuwasha mishumaa na kuwawekea maua waathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa hafla hiyo.
Azimio inasema hadi sasa, vifo 50 vimeripotiwa huku mamia ya wengine wakijeruhiwa na wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya.
Idadi rasmi ya waliouawa katika machafuko hayo haijatolewa na serikali .
"Azimio imefanya uamuzi kwamba Jumatano, badala ya kwenda mitaani kwa maandamano ya amani kama ilivyotangazwa hapo awali, tutafanya maandamano ya mshikamano na mkesha kwa wahasiriwa wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali katika maeneo yote ya nchi," ilisema taarifa hiyo.
"Tunawahimiza Wakenya wajitokeze kuwasha mishumaa na kuweka maua katika kuwakumbuka na kuwaheshimu waathiriwa. ... tunawahimiza Wakenya kusali na kusoma majina ya waathiriwa wa ukatili wa polisi. Tutatoa orodha ya waathiriwa kwa wakati kwa ajili ya zoezi hilo."