Soma hii kutoka TCRA

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema imezifungia laini za simu milioni sita kutokana na kutosajiliwa kwa alama za vidole.


Hata hivyo, baada ya kuzifungia laini hizo, laini milioni mbili kati ya hizo zimefunguliwa baada ya kusajiliwa kwa alama za vidole.

Kadhalika, mamlaka hiyo imesema hadi sasa jumla ya laini za simu milioni 33 sawa na zaidi ya asilimia 74, zimeshasajiliwa kwa alama za vidole.

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya Siku ya Usalama Mtandaoni, yaliyowakutanisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu.

Alisema wanaendelea na kazi ya kuzuia mawasiliano kwa laini za simu zote ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole na baadaye watazifungia kama hawatazisajili.

Kilaba alisema wamejipa muda wa kuwasubiri waliokuwa wamiliki wa laini hizo, kuzisajili kwa alama za vidole na endapo watashindwa kufanya hivyo zitafungiwa kabisa.

Uzimaji wa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, ulianza Januari 20, mwaka huu na kazi hiyo inaendelea.

Kuhusu maadhimisho ya siku ya usalama mtandaoni, alisema ni mpango wa kitaifa ulioanzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kukuza matumizi bora na salama ya mtandao wa intaneti.

Alisema lengo ni kuhamasisha jamii kutekeleza majukumu yake ili kuhakikisha uwapo wa usalama wa anga la mtandao dhidi ya matukio hatarishi ya kiusalama.

“TCRA imeiingiza siku hii kuwa moja ya mikakati ya kukuza ufahamu kuhusu usalama mtandaoni. Mkakati huu unalenga kuwezesha watumiaji wa mtandao wa intaneti nchini kufahamu majanga yaliyopo na njia mbalimbali za kujilinda ili kujiepusha na vitendo vya uhalifu mitandaoni pamoja na matumizi yasiyofaa ya mtandao wa intaneti,” alisema Kilaba.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu inasema ‘Pamoja kwa Mtandao Bora’, hivyo, Watanzania wote wana jukumu la kushirikiana kuhakikisha anga la mtandao linakuwa mahali salama kwa watu wa rika zote.

Post a Comment

Previous Post Next Post