Je unajiuliza uanze wapi ili kufikia ndoto zako za maisha ya kimataifa iwe kufanya kazi nje ya nchi, au kuwa na ushirikiano na watu wa mataifa mbalimbali. Katika makala hii naeleza mambo ya msingi ya kuzingatia ili uweze kuwa mshirika wa jumuiya ya kimataifa yaani uweze kuwa na marafiki na washirika toka mataifa mbalimbali katika shughuli zako halali za kila siku. Mambo haya ninayoeleza ni kwa uzoefu wangu na kujifunza toka kwa watu wengine, kitu tunachoita international exposure, yaani uzoefu wa kimataifa kwa kutembea na kuishi nchi tofauti tofauti.
Tamaduni za kuacha:
Kuna mambo kadhaa umejizoesha kuyafanya na ingawa twajua wazi si sahihi na yanakera wengine bado tunaendelea kuyafanya kwa kisingizio tuu eti hivyo ndivyo tulivyo. Ninasema twajua yanakera kwakuwa sisi tukifanyiwa mambo hayo hayo yanatukera. Mfano endapo utamuambia mtu utafanya kitu fulani, kisha usifanye kwa sababu fulani pengine ya kusahau au kutotilia maanani, wajua wazi kua hata wewe usingependa kutegemea jambo toka kwa mtu halafu mtu huyo asikufanyie.
Katika maisha ya kimataifa , ustaarabu ni kuthamini muda wa wengine, ni kuwajali wengine na kufanya mambo unayoahidi utafanya. Na kama hautoweza kufanya, basi utoe taarifa kwa wakati muafaka kuwa hautoweza.
Kuwa muwazi, mkweli na kuwajibika katika jukumu unalotarajiwa kufanya ni mambo yanayotarajiwa kutoka kwako ili uweze kufiti kuishi na watu wa mataifa tofauti wenye kuweza kushirikiana nawe kufika mbali kimaisha.
Uwezo wa kufikiri kwa akili ya kawaida na kubadilika
Kuna mambo mengi tunaamini na kufuata bila kufikiria sisi wenyewe. Pengine unafuata na kuamini mambo fulani sababu tuu ulisoma hivyo darasani, watu wengi wanaamini hivyo basi itakuwa ni sahihi, au kwakuwa watu fulani wenye vyeo, watu maarufu wa wakubwa kwako ki umri wanasema hivyo. Uwezo wako kuwa salama na kufanikiwa katika maisha ya kimataifa unahitaji sana uwezo wako binafsi wa kufikiri na kufanya maamuzi kwa kupima maelezo kwa akili yako ya kawaida tuu (common sense).
Utakutana na watu wengi wenye malengo tofauti hivyo utapata mitazamo na taarifa tofauti. Hautotakiwa kuamini zote, utatakiwa kuchuja wewe mwenyewe na kufanya maamuzi yenye manufaa kwako. Jifunze sasa kuhoji mambo, chunguza maamuzi yako na ujihoji hadi wewe mwenyewe . Tafuta taarifa zaidi ya unayoamini kuwa ni ukweli, unayosikia, na ukubali kuwa tayari kubadilika kimtazamo endapo utakuta kuwa ulichokuwa ukidhani ni sahihi sikuzote kumbe sio.
Uwezo wa kufanya mawasiliano
Nimeongelea sana umuhimu wa kujua kufanya mawasiliano kwa ufasaha na namna ya kufanya mawasiliano katika makala FANYA HIVI KAMA UNATAKA KUPATA UFADHILI WA MASOMO AU MTAJI WA BIASHARA Tafadhali bofya HAPA kusoma makala hiyo.
Ujuzi wa lugha
Pointi hii haihitaji maelezo kufafanuliwa sana kwani bila ujuzi wa lugha ya mawasiliano, hakuna kitu utaweza kufanya katika ulimwengu wa kimataifa, haijalishi uwezo wako wa kielimu, au bidii zako kikazi. Fahamu lugha kuu ya mawasiliano yaani Kiingereza.
Umuhimu wa ndoto
Ninaposema ndoto ninamanisha uwezo wako wa kufikiria na kutumaini mambo makubwa, sio ndoto zile za usingizini. Uwepo wa ndoto unakufanya utengeneze mwelekeo wa namna gani maisha yako unatakiwa uyaendeshe sasa ili kufikia huko unapotaka kuenda. Mfano kama unaota kuwa siku moja uende kufanya kazi nje ya nchi, basi bila shaka utaanza sasa kujifikiria namna gani ya kujiimarisha katika lugha ya kigeni na pia kuanza juhudi za kupata taarifa zaidi kuhusu maisha nje ya bongo. Usipokua na ndoto, basi utajichukulia poa na hivyo kutofanya juhudi sana.
Kuwa karibu na mtandao (Internet)
Matumizi ya mtandao ni zaidi ya kutumia Facebook , Instagrams, Blogs na WhatsApp. Baadhi ya watu huishia kutumia simu zao kwa ajili ya mitandao ya kijamii, na wakizidi sana watatumia Google kutafuta taarifa fulani. Maisha ya kimataifa yanakuhitaji uwe na uzoefu na taarifa tofauti tofauti nyingi kuhusu mataifa –siasa , uchumi, tamaduni, teknolojia na matukio makubwa. Na zaidi sana uwe na taarifa sahihi au zinatoka kwa vyombo huru na vya kuaminika na sio toka kwa watu wanao copy na kupaste kwa blogs zao au kwa akaunti zao za FB bila kufanya utafiti.
Kuwa na taarifa sahihi na kuzashare kunakufanya uaminike na kuonekana mtu sahihi wa kushirikiana katika mazungumzo.
Pia jizoeshe kutumia email kwa mawasiliano na mara kwa mara ufungue na kutumia akaunti yako ya email.