1. Usuli

Jioni
ya Ijumaa ya tarehe 13.8.1925, huku mvua kubwà na radi kali zikirindima
kijijini Kwambe, wilayani Mbinga, Mkoani Ruvuma, alizaliwa mtoto wa
kiume akiwa buheri wa afya. Wazazi wa mtoto huyo, Rev. DAVID KAMBONA na
Bi. MARIAM KAMBONA, wakampa mtoto huyo jina la OSCAR SATHIEL DAVID
KAMBONA. Mvua na radi hiyo, kwa mujibu wa mila za kijijini hapo, "nyumbi
hii, bombi hii", ilikuwa ni baraka na ishara kuwa mtoto huyo
atakujakuwa wa kipekee.
2. Elimu Chini ya Mwembe
KAMBONA,
tofauti na watoto wengine, hakusomea shuleni elimu ya awali bali
alifundishwa na wazazi wake pamoja na mjomba wake ambao wote walikuwa
walimu. Mafunzo hayo ya awali yalikuwa yakifanyika chini ya mwembe huku
chai na mihogo vikiwa pembeni.
3. Elimu ya "Middle School"
Baadae
KAMBONA alipelekwa shule ya Kati ya Mt. Barnabas, Liuli. Akiwa shuleni
hapo, KAMBONA alikuwa kipanga na "aliwatimulia vumbi" wanafunzi wote kwa
miaka yote alipokuwa shuleni hapo.
4. Alliance Sec. School
KAMBONA
alifaulu vizuri mitihani yake na akachaguliwa kujiunga na "Alliance
Sec. School", Idodomia ambayo baadae ikajaitwa Mazengo Sec. School.
Almanusra KAMBONA asiendelee na masomo kwani baba yake hakuwa na uwezo
wa kulipa £ 30 kwa mwaka. Uwezo wa KAMBONA "kutema yai" ndio uliomponya
kwani alifanikiwa kumshawishi Askofu kumlipia ada hiyo baada ya kusali
Sala ya Baba Yetu kwa Kiingereza!.
5. Tabora Boyz Sec. School
KAMBONA
alisoma shule hii pamoja na J. Lusinde, E. Mzena, B. Ngwilulupi, A.
Nsekela, A. Nyirenda na K. Chiume. Ni akiwa shuleni hapo ndipo kwa mara
ya kwanza, KAMBONA alionana na NYERERE aliyekuwa akifundisha St. Marys,
Tabora.
6. Ualimu Alliance Sec. School
Baadae, KAMBONA alienda kufundisha shule hii na akakutana na J. Lusinde na K. Chiume na baadae akawa "Schoolmaster".
7. KAMBONA akutana na NYERERE tena
KAMBONA alikutana na NYERERE kwa mara ya 2 kwenye Mkutano wa taifa wa waalimu mwaka 1954.
8. KAMBONA Ajiunga TANU
Mwaka
1955, KAMBONA alijiunga na TANU iliyozaliwa tarehe 7.7.1954 na akaonesha
bidii kubwa huku akifanya kazi kwa kujitolea kwani TANU haikuwa na
fedha. Bidii yake ilipelekea kuwa Katibu Mkuu wa TANU.
9. KAMBONA Awaingiza TANU Watanganyika 100,000
KAMBONA
alitembea nchi nzima kwa miezi 6 akionana na Machifu na wanavijiji na
kufanikiwa kuingiza wanachama 10,000. Baadae akiendelea na harakati hizo
na baada ya miezi 12 akawa ameingiza wanachama 100,000. Viongozi
wenzake wa TANU walimpongeza sana kwani TANU ikawa inaenea kwa kasi
sana.
10. KAMBONA Afungua Akaunti ya Kwanza ya TANU
KAMBONA
alikuwa na mawazo ya kimaendeleo kwani kutokana na michango ya
wanachama aliweza kufungua akaunti ya kwanza ya TANU. Kwa hakika, hili
lilikuwa ni jambo la kihistoria.
11. KAMBONA afuma "Governor's Scholarship" kusomea Sheria, UK
Mwaka 1957, KAMBONA alipata fursa ya kwenda UK kusomea LLB kwa miaka 3 na hivyo akaenda huko.
12. KAMBONA Awa Mtangazaji wa 1 wa Kiswahili BBC 1957
Tarehe
27.6.1957, KAMBONA aliweka historia kwa kutangaza Kiswahili BBC kwa
mara ya 1 akisema-: "Hapa ni London, kwa mara ya kwanza BBC inawaletea
habari kwa Kiswahili wananchi wa Afrika Mashariki. Asalaam Aleikhum".
13. KAMBONA awa Mwenyekiti wa TANU London
Kutokana
na talanta yake kubwa ya uongozi, KAMBONA alichaguliwa kuwa Kiongozi wa
wanafunzi chuoni na Mwenyekiti wa Tawi la TANU, London.
14. KAMBONA na NYERERE Washeachumba Chuoni London
Kati
ya tarehe 26.6.1959 na 7.8.1959, NYERERE alikwenda UK kwa matayarisho ya
uhuru wa Tanganyika na akalala chumba kimoja na KAMBONA ambaye walikuwa
"wameshibana" sana. Katika "Press Conference" ya 1991 KAMBONA alisema-
"TANU haikuwa na hela hivyo ili kubana matumizi, nikakaa na NYERERE room
yangu chuoni na hii ilisaidia tuwe na muda mwingi wa majadiliano".
15. KAMBONA Amuoa MISS Tanganyika
Tarehe
19.11.1960, KAMBONA alimuoa Miss Tanganyika mrembo, Bi. FLORA MORIYO
toka Kilimanjaro. Harusi hiyo ya kukata na shoka ilifanyika St. Paul
Cathedral, London na kuhudhuriwa na wageni waalikwa 400. NYERERE alikuwa
ndiye msimamizi aliyemsindikiza Bi. FLORA altareni. Ilikuwa ni harusi
ya kwanza ya watu weusi kanisani hapo na ilitoka kwenye magazeti
mbalimbali ya Ulaya.
16. KAMBONA Arejea Bongo
KAMBONA alirejea Bongo kuendelea na harakati za uhuru akihudumu kama Waziri wa Elimu na Katibu Mkuu wa TANU.
17. KAMBONA Awa Waziri wa 1 wa Mambo ya Nje
Katika Baraza la kwanza la Mawaziri la Tanganyika, KAMBONA aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi.
18. KAMBONA Kipenzi cha 2 cha Wananchi baada ya NYERERE
KAMBONA
alipendwa sana nchini kwani alikuwa msomi, mwanasiasa hodari,
mtanashati na vijana wengi walimuiga staili yake ya nywele "KAMBONA
Style". Kwa hakika, KAMBONA alipendwa sana.
19. KAMBONA- Kiongozi PEKEE Aliyewakabili Waasi, 1964
Usiku
wa tarehe 19.1.1964, askari wa kambi ya Colito(Lugalo) waliasi wakidai
marupurupu na nafasi za juu za vyeo kwa Waafrika. Rais NYERERE na Mh.
RASHID MFAUME KAWAWA walitoroshwa na mlinzi wao, PETER BWIMBWO usiku wa
manani hadi Kigamboni na kufichwa kwenye nyumbaya Mzee KIZWEZWE.
Mawaziri
wote walibanisha makwao baada ya kupigiwa simu na Mh. J. LUSINDE,
Waziri wa Mambo ya Ndani, kuhofia usalama wao. KAMBONA ndiye pekee
aliyeingia "fronti" kwani si tu raia waliokuwa wakimpenda bali pia
askari. Waasi walionekana kutulia baada ya mambo yao kuwekwa sawa lakini
baada ya Rais NYERERE kuibukia Ikulu toka mafichoni baada ya siku 3,
waasi "wakalianzisha" tena hivyo ikabidi maasi hayo yalizimwe kwa msaada
wa Waingereza na baadae Wanaijeria.
20. KAMBONA Ashuhudia mchakato wa Muungano 1964
KAMBONA
alikuwa ni mmoja wa mawaziri wachache sana waliokuwa wakijua mchakato
wote wa muungano kwa undani na pia alishuhudia utiaji saini hati za
muungano huko Zenji, tarehe 22.4.1964 kati ya Rais NYERERE na Rais wa
Zanzibar, Mh. ABEID AMAN KARUME.
21. KAMBONA Atofautiana na NYERERE Mfumo wa Chama Kimoja
Baada
ya ziara ya China 1965, NYERERE alivutiwa na "alikuwaameoza" kwa siasa
za China na mfumo wao wa siasa hivyo akaunda Tume tarehe 28.1.1964 ili
ipendekeze mfumo gani unaifaa nchi yetu. Tume hiyo ilikuwa chini ya Mh.
KAWAWA ikapendekeza mfumo wa chama kimoja. KAMBONA, ambaye daima alikuwa
hapepesi macho wala hayumbishwi, aliweka kunji na kutosaini ripoti hiyo
na badala yake akatayarisha ripoti yake ya kutaka mfumo wa vyama vingi
na NYERERE akahuzunishwa sana na msimamo huo wa KAMBONA.
Kipindi hiki NYERERE aliishamuondoa KAMBONA kwenye wizara zile nyeti.
22. NYERERE "Amchana" kiaina KAMBONA 77 ya 1966
Tarehe
7.7.1966, NYERERE, akihutubia Taifa katika sherehe za 77, NYERERE
alitumia mafumbo "kumpa za uso" KAMBONA ambapo alisema viongozi
wanaonekana kujipatia mali nyingi kiajabu hawafai hata kidogo.
23. KAMBONA Ajiuzulu u-Waziri na U-Katibu Mkuu TANU 1967
Tarehe
9.6.1967, KAMBONA alibwaga manyanga kwa kujiuzulu U-Katibu Mkuu wa TANU
na Uwaziri wa Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini ambapo alitaja
sababu za kiafya kuwa ndizo zilipelekea achukue uamuzi huo.
24. KAMBONA Atorokea Kenya, 1967 ki-James Bond !!
Kwakuwa KAMBONA alikuwa ni mtoto wa mjini, alitonywa kwamba kuna mpango wa kumkamata na kumsweka kizuizini.
Hivyo,
usiku wa kuamkia tarehe 26.7.1967, KAMBONA, mkewe, watoto wake 2 na
msaidizi wa kazi walifunga virago na ku-drive hadi Kenya kwa staili ya
"James Bond"! Watu wengi walipigwa butwaa ni kwq vipi aliweza kutoroka
bila kubambwa!.
Usiku
wa siku hiyo jijini Nairobi, KAMBONA na familia yake walikwea "pipa"
East African Airways Flight 720 kwenda "Kwa Mama, huku, huku nyuma
ikadaiwa alitoroka na mamilioni ya fedha!.
25. NYERERE Aelezea "Kusepa" kwa KAMBONA
Siku
chache baada ya KAMBONA "kula kona", NYERERE, akiongea na viongozi wa
TANU Morogoro, alisema : "Itachukua muda mrefu kufahamu sababu za Bw.
KAMBONA kujiuzulu, lakini jambo moja ni dhahiri; KAMBONA amenidanganya
mimi, TANU, TZ na Afrika".
26. KAMBONA Ajitetea UK
Baada
ya kusikia vijineno kwamba amesepa na mamilioni, tarehe 6.9.1967,
KAMBONA alikanusha vikali na kuitaka serikali ya Tanzania iwasiliane na
ya Kenya kupata uthibitisho kitu ambacho serikali ya TZ hakikufanyika.
27. OTTIN na MATTIYA KAMBONA "Wasukumiziwa Ndani",1967
Hawa wadogo zake KAMBONA walionja "joto ya jiwe" kwani walinyakwa usiku tarehe 30.12.1967 na kuwekwa kizuizini, Ukonga.
Familia
zao zikasambaratika vibaya sana kufuatia kukamatwa kwao. OTTIN alikuwa
ni "Journalist" na MATTIYA alikuwa mfanyakazi Wizara ya Kilimo. OTTIN
alikuwa amemuoa raia wa Martinique na walikuwa na watoto 2 wadogo na
MATTIYA alikuwa amemuoa Mgambia wakiwa na mtoto wa miezi 3 tu. Wanawake
hao walifukuziliwa mbali na kurudishwa makwao pamoja na watoto wao!.
28. KAWAWA "Amchana" KAMBONA Bungeni, 1968
Jumanne ya tarehe 23.1.1968, KAWAWA, 2nd VP, alilitaarifu Bunge:
"Wote
mnajua kwamba Bw. KAMBONA aliikimbia nchi mwaka jana, 1967. Kabla
hajaondoka, tarehe 6.12.1966, TZS 500.000/= ziliingizwa kwenye akaunti
yake toka benki moja ya Uingereza. Uchunguzi wa BOT toka KAMBONA atoroke
umeonesha kuwa tangu Juni 1965 na Desemba 1966, KAMBONA aliingiza
katika akaunti yake jijini Dsm TZS 896,800/=. Kambona pia alikuwa
anamiliki majumba mengi (Nyumba Magomeni-Plot No. 21,39 31), (Kunduchi
bichi-Plot No.28), (Msasani bichi -Plot No. 92), (Morogoro-Plot No. 89)
ns (Songea-Plot No.21)".
29. KAMBONA Amchana NYERERE nchini Nigeria, 1968
Baada
ya TZ kuitambua Biafra, serikali ya Rais YAKUB GOWON ilikasirishwa sana
hivyo ilimwalika KAMBONA aichafue TZ . Kwahakika, "jipu likawa limepata
mkunaji" Hivyo, KAMBONA akaenda na kutoa muadhara Lagos tarehe 14.6.1968
ambapo "alimchana" vilivyo Rais NYERERE na kumwita dikteta. KAMBONA
akaonesha kukosa uzalendo kwa taifa lake pale alipozomoka, bila
ushahidi, kwamba TZ imepeleka vifaa vya kijeshi Biafra badala ya
Zimbabwe!.
30. TANU "Yamfyekelea mbali" KAMBONA
NEC ya
TANU iliyokuwa ikiketi Tanga, tarehe 19.10.1968, ilimvua uanachama
KAMBONA pamoja na wabunge wengine 8 "Vichwa-maji" waliohoji uhalali wa
TANU kuwa juu ya Bunge. Wabunge hao ni W. Mwakitwange, M. Choga, S.
Kibuga, J. Bakampenja, E. Anangisye, G. Kaneno na Dr. F. Masha.
31. NYERERE "Amchana" tena KAMBONA, 1969
Tarehe 12.1.1969 kwenye sherehe za Mapinduzi Znz, NYERERE "alimuwakia" KAMBONA na kusema- "KAMBONA ni mwizi na mhuni kisiasa.
32. KAMBONA Akejeliwa Mashuleni na Majeshini
Nyimbo nyingi za kumkejeli KAMBONA zilitungwa majeshini na mashuleni lakini zilizokuwa maarufu ni hizi 2:
1. KAOMBONA Kaolewa wapi....? Kwa Wazungu...Kisa nini?...Tamaa ya Mali!
2. Alimselema ...alija, akija KAMBONA chinja... chinjilia mbali..!!.
33. KAMBONA Adaiwa ni _"Mastermind"_wa Uhaini, 1969
Mwaka
1969, KAMBONA alidaiwa kuwa "Mastermind" wa uhaini. Mashitaka yalikuwa
kwamba washtakiwa 7 wakishirikiana na KAMBONA kati ya Machi 1968 na
Octoba 1969, walitaka kumuua Rais NYERERE na kuipindua serikali.
Washtakiwa hao 7 ni (Bibi Titi Mohamed , Michael Kamaliza, Gray
Mattaka, John na Eliya Chipaka, Capt A. Milinga na W. Chacha).
Kesi
ilianza kurindima Jumatatu tarehe 6.6.1970 na ilisikilizwa na Jaji Mkuu
Georges na iliendeshwa na AG Mark Bomani. Wanafunzi wa Sekondari
Tambaza(F.V Arts akiwepo Othman Chande, Jaji Mkuu wa 7) walikuwa
wakijongo vipindi kwenda kortin kushuhudia kesi hii iliyokuwa na mvuto
wa aina yake.
Washtakiwa
wote walitiwa hatiani kasoro A. Milinga na KAMBONA ambaye hakuwepo. M.
Kamaliza na mwenzake walipigwa "mvua" 10 na wengine walifungwa maisha
na Bibi Titi akapata msamaha 1972.
34. OTTIN MATTIYA Waachiwa 1978
Tarehe
5.2.1978, katika kusheherekea mwaka 1 wa kuzaliwa CCM, NYERERE,
akitumia ibaracya 45 ya Katiba, aliwaachia huru OTTIN na MATTIYA pamoja
na JOSEPH KASELABANTU( Mwasisi wa TANU).
OTTIN
na MATTIYA, baada ya kugundua familia zao hazipo, wakaona Bongo hamna
ishu nao wakaamua pia kusepa. Walivuka mpaka wa TZ na Kenya usiku
Kininja kwani mpaka huo ulikuwa umefungwa kutokana na uhasama bainavya
TZ na Kenya na wakaelekea UK.
35. NYERERE NA KAMBONA walikuwa majirani Msasani
Baada
ya KAMBONA kuondoka nchini 1967, nyumba yake ikawa inakaliwa na Rais
MILTON OBOTE kwa takribani miaka 10 baada ya kupinduliwa na Nduli IDD
AMIN, 1971.
36. Vyama Vingi vyaanzishwa Bongo, KAMBONA ataka kurejea
Baada
ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa mwaka 1992, KAMBONA akiwa London
alisema, ije mvua, lije jua, anarejea kwenye Taifa lake. Serikali
ikamuonya kuwa asithubutu na akijifanya fyatu au kichwa-maji akatia pua
yake tu Bongo, "hakuna rangi ataacha kuiona".
37. KAMBONA Aitunishia msuli serikali, Atinga Bongo
KAMBONA
aliamua kuwa kama "Mbwai, mbwai tu" hivyo akaonesha "Shoo za kibabe" na
kurejea nchini akisafiria nyaraka za Umoja wa Mataifa zilizotolewa na
serikali ya UK. Aliporejea hakukamatwa na badala yake, tarehe 4.9.1992,
serikali ilimpa miezi 3 aweke sawa uraia wake kwakuwa ni Mmalawi! Miezi
hiyo iliisha tarehe 4.12.1992 na serikali "ikaufyata" kwani haikumfanya
kitu chochote!.
38. KAMBONA aeleza sababu za kutoroka, 1967:
Baada ya kurejea nchini, KAMBONA alikata kiu ya wote waliotaka kujua kilichopelekea asepe "Kwa Mama" ni nini ambapo alitiririka:
"Mimi
na NYERERE tumetoka mbali. Sisi ndio tuliokuwa Viongozi wakuu wa TANU;
Yeye Mwenyekiti, mimi Katibu Mkuu. NYERERE aliporudi toka China 1965
alitaka kuleta sera za China na mfumo wa chama kimoja. Nikapingana
nae.."
39. KAMBONA Aeleza alichokuwa akifanya UK
Wiki 2
baada ya kurejea nchini, KAMBONA alitiririka kitu alichokuwa akifanya
nchini Uingereza kwa miaka 25 aliyoishi huko ambapo alisema- "I did
business. I used to go to the Arab countries but this did not last. I
then depended on income support from Britain. Every Tuesday You take
your book to the Post office...
40. KAMBONA atishia "Kumwaga ugali na mboga" kuhusu NYERERE
Badala
ya kushugulikia uraia, KAMBONA akaendeleza bifu lake na NYERERE ambapo
alisema anataka kufanya mkutano mkubwa viwanja vya Jangwani ili aeleze
ufisadi wa NYERERE. Mapadri na masheikh walimsihi sana lakini
akashikilia msimamo wake.
41. KAMBONA Ambwelambwela Jangwani,1992
Tarehe
21.11.1992, viwanja vya Jangwani viliweka rekodi kutokana na umati
mkubwa wa "wapenda ubuyu" uliojitokeza toka mida ya mchana kulisikia
Jabali hilo litaeleza nini kuhusu Baba wa Taifa, Mwalimu NYERERERE.
KAMBONA
aliwaboa sana 90% ya waliohudhuria kwani alidai, bila ushahidi, kuwa
NYERERE, AMIR JAMAL na KAWAWA wameficha mamilioni ya fedha mabenki ya
Ulaya. KAMBONA akaenda mbali na kudai NYERERE ni Mtutsi, KAWAWA na MKAPA
ni watu wa Msumbiji na MALECELA ni Mcongoman!. Ikaonekana ni hekaya za
Abunuwasi na hadithi za Esopo tu!.
42. NYERERE Amjibu KAMBONA
NYERERE,
siku chache baadaye akiwa Msasani, aling'aka- "Mimi ni lofa. I dont
have a single penny abroad, I can assure you. Kama RASHID na AMIR
hawawekwi kundi la watu waaminifu duniani, labda neno uaminifu ni neno
tu, halina maana. Hawa ni waaminifu sana. Pia, mimi sipendi kuhusishwa
na mambo ya kijingajinga. Ni makosa kushindana na kundi la wapumbavu.
Kambona alete ushahidi maana "any blessed fool could stand up there" na
kusema chochote".
43. MAWAKILI wamchimba Mkwara-Mbuzi KAMBONA
Baada
ya KAMBONA kutoa kashfa dhidi ya viongozi hao mashuhuri nchini, mawakili
wa Viongozi hao walimpa siku 14 toka tarehe 8.12.1992 kuomba radhi au
kutoa ushahidi.
KAMBONA
aliwajibu kuwa _"Mtu mzima hatishiwi nyau"_na akachekesha watu pale
alipodai _"Nondo" zake kuhusu "bank accounts" za viongozi hao amezisahau
UK!.
44. KAMBONA Aunda TADEA
KAMBONA aliunda chama cha TADEA ambacho hakikuleta upinzani wowote wa maana.
45. KAMBONA afariki London, 1997
KAMBONA
alifariki jijini London mwaka 1997 na mwili wake kuletwa nchini na
kupokelewa na ndugu zake na kiongozi wa serikali, Mh. J.M. KIKWETE,
Waziri wa Mambo ya Nje. Rafiki yake NYERERE hawakuwahi kuonana toka
atoroke mwaka 1967 na wala hakwenda kwenye mazishi yake.
46. RAIS KIKWETE Akutana na Mke wa KAMBONA, 2007
Tarehe
28.6.2007 katika hotel ya Kilimanjaro Kempisk, Rais wa awamu ya nne,
Mh. JK alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za miaka 50 ya BBC KISWAHILI.
Mh. JK, akiwa na mcheshi na mwenye bashasha kama kawaida yake, alikutana
na kusalimiana na Bi. FLORA KAMBONA ambaye alikuwa mgeni mahsusi kwani
mmewe, KAMBONA ndiye aliyekuwa Mtangazaji wa 1 wa BBC Kiswahili, 1957.
46. MWISHO:
Huyu ndiye OSCAR SATIEL DAVID KAMBONA aliyekuwa chanda na pete na Mwalimu NYERERE lakini mwisho wakawa maadui wasio na mfanowe!.
Tafakuri Tunduizi:
ATIKALI HII YA KUKATA NA SHOKA ina Tafakuri Tunduizi 100!!!
Tags
MAKALA


