Vyanzo vya kiintelijensia nchini Kenya vinaashiria madaktari wawili wa Cuba waliotekwa mjini Mandera Kaskazini Mashariki mwa Kenya mwezi Aprili wamelazimishwa na wanamgambo wa al-Shabab kujiunga na dini ya Kiislamu.
Mtandao wa gazeti la Daily Nation umenukuu ripoti ya kiusalama ya hivi karibuni ya ukisema kuwa madaktari hao wamehamishiwa katika msitu wa Halaanqo karibu na mji wa Barawe Kusini Magharibi mwa Somalia ambako wanadaiwa kuwasilimisha kwa lazima.
Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya Hilary Mutyambai amesema oparesheni ya ukombozi wa madaktari hao raia wa Cuba inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kupata idhini ya kuvuka mpaka wa Kenya na Somalia.
"Kazi yetu kama polisi inaishia mpakani ... siko katika nafasi ya kuelezea hatma ya madaktari wa Cuba waliotekwa lakini maafisa wangu wanashughulikia," alisema Bw. Mutyabai akielezea changamoto inayowakabili mafisa wake.
Hata hivyo Mutyambai aligusia kuwa wanawazuilia baadhi ya wahukiwa ambao wanasaidia katika shughuli ya uchunguzi.
Madaktari hao walivyotekwa
Watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki waliwateka madaktari Assel Herera Corea na Landy Rodriguez, mwezi Aprili katika uvamizi mkali ambapo mmoja wa afisa wawili wa polisi waliokuwa wakiwasindikiza madaktari hao katika kituo chao cha kazi alipigwa risasi na kuuawa.
Watekaji hao walioshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab, baadae waliitisha dola elfu 150 kama kikombozi, kwa mujibu wa wazee wa kijamii walioenda kijiji kimoja kushiriki katika mazungumzo ya kushinikiza kuachiliwa kwaokatika eneo la Jubbaland, Somalia.
Hatma ya madaktari hao wa kigeni haijulikani kufikia sasa.
Inaarifiwa madaktari hao wanaishi karibu na makaazi ya Gavana wa eneo hilo ambayo ni kilomita takriban 4 kutoka eneo la mpaka na Somalia.
Haijulikani ni washambuliaji wangapi waliokuwa ndani ya magari aina ya Probox ambayo kwa mujibu wa duru yalikuwa yameegeshwa karibu na makaazi hayo.