Msomi na mwanasiasa wa Kenya Dkt Reuben Savai, 70, ambaye jaribio lake la kuwania kiti cha urais mwaka 1997 na 2002 lilitibuka amefariki.
Mwanawe wa kiume Daniel Lihanda amenukuliwa na Gazeti la Daily Nation nchini Kenya, akithibitisha kifo chake siku ya Jumapili.
Licha ya kuwa na shahada sita na cheti cha diploma, mwanasiasa huyo mwenye utata hakuwahi kupata kazi nchini Kenya.
Dkt Savai, ambaye alisomea shahada sita nchini Ugiriki na diploma kutoka Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, juhudi zakiongozi huyo wa chama cha Kenya Republican Reformation Party kupata kazi Kenya ziligonga mwamba.
Baadhi ya vitu alivyosomea ni pamoja na Diploma ya Thiolojia, Shahada moja ya sheria, shahada mbili za elimu na nyingine moja ya Sayansi.
Familia yake inasema alizuiliwa kufanya kazi ya sheria nchini Kenya kwa sababu hakufuzu katika chuo cha mafunzo ya sheria nchini humo.
Dkt Savai, ambaye alitaka kuwampinga marais wastaafu wa Kenya Daniel arap Moi na Mwai Kibaki, alizuiliwa kuwania kiti cha urais kwa kukosa stakabadhi zilizohitajika kuidhinishwa kuushiriki chaguzi hizo
Miaka ya 1990, alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha Forum of Restoration and Democracy (Ford), Kenya iliporejelea siasa ya vyama vingi.
Mwaka 1997, Dkt Savai aliwania kiti cha ubunge na cha lang'ata lakini alishindwa na Raila Odinga, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa chama cha National Development Party (NDP).
Eneo bunge la Lang'ata liligawanywa mara mbili- Lang'ata na Kibra - kufuatia uhakiki wa mipaka kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2013.
Bw Lihanda aliliambia gazeti la Nation kuwa baba yake alipatikana amefariki nyumbani kwao katika kile kinachoshukiwa kuwa kupooza.
Lihanda anasema baba yake hakuwahi kuajiriwa nchini Kenya licha ya kisomo kikubwa alichokuwa nacho na kujihusisha kwake katika siasa za nchi hiyo.
Umasikini
"Alisomea ulaya na kupata shahada sita na na cheti cha Diploma. Aliporudi Kenya hakuwahi kupata kazi akaamua kujitosa katika siasa'' alisema Lihanda.
Aliongeza kuwa baba yake alikuwa akisumbuliwa na tattizo la shinikizo la damu licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Familia ya mwanasiasa huyo sasa inatoa wito kwa wahisani kuisaidia kuchangisha dola 1,274 kugharamia mazishi yake.
Mwili wake umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi wafu mjini Kaimosi Magharibi mya Kenya.