BUNGE LAPIGA MARUFUKU MAKAHABA

Nairobi

Nairobi, Kenya. Bunge la Kaunti ya Nairobi nchini Kenya limepitisha kwa kauli moja hoja ya kupiga marufuku makahaba kuendesha biashara zao jijini humo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya wawakilishi hao kulalamikia juu ya kuongezeka kwa biashara ya ngono jijini Nairobi.

“Makahaba wameongezeka sana Nairobi katika muda wa miaka kadhaa iliyopita. Wamekuwa wengi sana katika maeneo mengi Nairobi,” amesema mwakilishi wa eneo la Woodley Kenyatta Golf Course, Abraham Njihia.

Njihia amesema ukahaba unafanywa wazi na kutaka wakiukaji kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Kifungu cha 63 sehemu ya 153 na 154, cha sheria za Kenya kimekataza ukahaba kikisema wanawake na wanaume kushiriki ngono kwa lengo la kujinufaisha kifedha ni kitendo kisichokubalika.

Mwakilishi maalum wa ODM, Mellab Atema ambaye aliunga mkono mswada huo amesema ukahaba unamaliza utamaduni wa Kiafrika.

Amesema baadhi ya vijana wa mitaani walimwambia kuwa wakati mwingine ombaomba mitaani hufanya hivyo kwa lengo la kupata fedha za kulipia ngono. Viongozi hao wamesema majumba mengi ya ukahaba (madanguro) yamebandikwa kuwa ‘majumba ya kuchua mwili ili kuondoa uchovu’.

Walitaja eneo la Hurlingham, Yaya Centre na Adams Arcade kama maeneo yaliyo maarufu kwa madanguro hayo. Mwakilishi wa Wadi ya Imara Daima, Kennedy Obura amesema ukahaba unaanza baa ambako hakuna udhibiti wa umri.

“Kila kitu siku hizi ni mfumo wa kidijitali, wazazi walio kazini hawajui wanachofanya watoto wao nyumbani katika intaneti,” amesema.

Amesema cha kushangaza ni kuwa wengi wanaohusika ni wasomi ikiwamo wale wa vyuo vikuu. Mjadala huo unatarajiwa kuendelea Desemba 5.



Post a Comment

Previous Post Next Post