MGOMBEA WA CHADEMA APATA DHAMANA

Admin
By -
0


Mwanza. Mgombea udiwani Kata ya Mhandu (Chadema), Godfrey Misana amepata fursa ya kushiriki kampeni za lala salama za uchaguzi mdogo wa Novemba 26, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza kumwachia kwa dhamana katika shauri la kujeruhi linalomkabili.

Mgombea huyo pamoja na meneja wake wa kampeni, Charles Chinjibela na watu wengine wawili wanakabiliwa na kesi namba 540/2017 ya kumjeruhi meneja wa kampeni wa CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba katika tukio lililotokea Novemba 14.

Washitakiwa wengine waliounganishwa katika shauri hilo leo Jumanne ni Dominic Izengo na Ebenezer Mathew.

Katika uamuzi wake Hakimu Mkazi, Ainawe Moshi amesema baada ya hoja za pande zote na kupitia vifungu vya sheria, Mahakama inakubaliana na hoja za upande wa utetezi unaowakilishwa na mawakili Gasper Mwanaliela na Paul Kipeja kuwa shtaka hilo lina dhamana na upande wa Jamhuri haujatoa hoja za kuishawishi Mahakama kuzuia dhamana.

“Baada ya kusikiliza ombi la upande wa Jamhuri la kuzuia dhamana na hoja za upande wa utetezi kupinga ombi hilo, Mahakama imejiridhisha kuwa hakuna hoja zenye uzito katika macho ya sheria za kuendelea kuwashikilia mahabusu washtakiwa, hivyo inawaachia kwa dhamana,” amesema Hakimu Moshi katika maamuzi yake.

Awali, Wakili wa Serikali, Elizabeth Barabara ametumia kifungu cha 148 (a) (d), cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kuomba dhamana za washtakiwa kuzuia kwa alichodai ni usalama wao.

Hakimu Moshi ametaja sharti la dhamana kuwa ni kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh2 milioni kila mmoja. Shauri hilo limeahirisha hadi Desemba 7 mwaka itakapotajwa tena.


Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)