MEYA WA UBUNGO AACHIWA USIKU WA MANANE
By -
November 26, 2017
0
Dar es Salaam. Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ameachiwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa polisi kwa takriban saa 15 akidaiwa kutaka kupanga njama za vurugu baada ya matokeo ya udiwani wa Kata ya Saranga kutangazwa.
Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo (Chadema) alikamatwa na polisi jana Jumapili Novemba 26,2017 saa tano asubuhi katika kituo cha kupigia kura cha Mtakatifu Peter, Kimara.
Akizungumza na MCL Digital leo Jumatatu Novemba 27,2017 baada ya kuachiwa na polisi, Jacob amesema alipokamatwa alipelekwa vituo vya Mbezi kwa Yusuf, Mabatini na baadaye Oysterbay alikokaa muda mrefu.
"Nimeachiwa saa 7:40 usiku kwa dhamana, hizi zote zilikuwa ni njama za kutunyima ushindi. Dhamana gani inatolewa usiku?” amehoji Jacob.
Amesema, "Hii ilikuwa mipango ili Chadema isishinde ila wakazi wa Ubungo wasivunjike moyo na haya, wamejionea hali halisi iliyofanyika na huu ni ushindi kwetu."
Jacob ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amesema ametakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay leo.
Tags: