Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajiwa kuwahutubia wakazi wa Kata ya Mhandu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, mgombea wa chama hicho, Godfrey Misana yupo mahabusu kutokana na kukabiliwa na shtaka la kujeruhi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Boniphace Nkobe amesema Mbowe ameambatana na aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu.
Amesema mkutano huo pia utahudhuriwa na aliyekuwa mbuge wa Nyamagana, Ezekia Wenje na utafanyika saa kumi jioni.
Misana (46), mgombea udiwani wa Chadema katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26,2017 na kampeni meneja wake, Charles Chinjibela (37) Ijumaa Novemba 17,2017 walipandishwa kizimbani wakidaiwa kumjeruhi meneja wa kampeni za CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba.
Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, mbele ya hakimu Ainawe Moshi wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 14,2017.
Akisoma mashtaka katika shauri hilo namba 540/2017, mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Elizaberth Barabara alidai washtakiwa walitumia visu na mawe kumjeruhi Warioba.
Upande wa Jamhuri uliomba Mahakama kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa kile ilichoeleza ni kwa usalama wao.
Ombi hilo la Jamhuri limepingwa na wakili wa utetezi, Gasper Mwanaliela.
Wakili Mwanaliela alisema dhamana ni haki ya wateja wake na kwamba, kuwanyima kutawazuia kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaotarajiwa kufanyika Novemba 26,2017.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Moshi alisema Mahakama itatoa uamuzi kuhusu dhamana Novemba 21,2017. Washtakiwa walipelekwa mahabusu.
Post a Comment
0Comments
3/related/default