MAPYA YAIBUKA KIFO CHA MWANAFUNZI MKOANI KILIMANJARO

Admin
By -
0

 Mambo mapya yameibuka katikakifo cha mwanafunzi Humphrey Makundi (16) wa Shule ya Sekondari ya Scolastica iliyopo Himo baada ya mzazi kutuhumu kuwa mwanaye alipigwa.

Uchunguzi wa mwili wa mtoto huyo aliyekuwa kidato cha pili ulifanywa na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Mbali ya hilo, uongozi wa shule umeeleza namna ulivyobaini kutoweka kwa mwanafunzi huyo na hatua ulizochukua.

Baba wa mtoto huyo, Jackson Makundi aliliambia gazeti hili akiwa hospitali ya KCMC kuwa uchunguzi unaonyesha alipigwa.

“Uchunguzi umethibitisha alipigwa na kitu chenye ncha kali kikapasua fuvu. Inaonekana alikatwa na kitu chenye ncha kali kiunoni, mgongoni, kwenye mapaja na mbavu mbili zilivunjwa,” alisema Makundi aliyeshuhudia uchunguzi wa mwili wa mtoto wake.

Alisema ni dhahiri kifo cha mwanaye kinatia shaka, hivyo ni wajibu wa vyombo vya uchunguzi kuwatafuta wahusika.

Juzi, kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah alikataa kueleza kwa undani tukio hilo licha ya kuwepo madai kuwa mwanafunzi huyo alipigwa na mlinzi, akitaka polisi iachwe ichunguze.

“Yote mnayouliza ndiyo sehemu ya uchunguzi tunaoendelea nao. Tumeshafikia asilimia 50 katika uchunguzi wetu na tunawashikilia watu 11 akiwamo mmiliki wa shule,” alisema Kamanda Issah.

Akizungumzia tukio hilo, mkurugenzi wa Shule ya Scolastica, Elizabeth Shayo alisema mwanafunzi huyo alitoweka shuleni Novemba 7 kati ya saa 12:00 na saa 1:00 asubuhi na si Novemba 6 kama inavyoelezwa.

“Siku hiyo alimuaga head prefect (kaka mkuu) kuwa anakwenda KCMC kwa kuwa anaumwa jicho. Head prefect alijua atafuata utaratibu na wakati mwingine huwa wanasindikizwa na matroni,” alisema.

“Siku hiyo kulikuwa na quiz (jaribio) ya fizikia, lakini hakuonekana. Walimu wakajua labda ametoroka na angerudi kwa sababu suala la utoro kwa wanafunzi ni mambo yapo.”

Shayo alisema mwanafunzi hakuonekana na ilipofika saa 1:00 usiku uongozi wa shule uliitisha ‘roll call’ ndipo ikathibitika hayupo shule na Novemba 8 asubuhi mzazi wake alijulishwa. Alisema mkuu wa shule, Michael Shiloli aliyezungumza na mzazi, waliafikiana waendelee kumtafuta wakitarajia angerejea shuleni na baada ya kutorejea, walikubaiana kutoa taarifa polisi Novemba 10 na uongozi wa shule ukafanya hivyo kwa kutoa tangazo kanisani.

Shayo alisema matangazo hayo yalitolewa Novemba 11 katika Usharika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Himo na Kanisa Katoliki.

Alisema walipotoa taarifa kulikuwa na uvumi kuwa kuna mwili uliokotwa mtoni na ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi.

Shayo alisema alimtuma mkuu wa shule na mwalimu wa darasa kwenda chumba cha kuhifadhi maiti Mawenzi ili kutambua mwili huo.

Alisema walipokwenda mhudumu wa mochwari aliwaeleza walishauzika mwili huo na si wa mtoto bali ni wa mtu mzima anayekadiriwa kuwa na miaka 35, kauli iliyotolewa pia na polisi.

Shayo alisema Novemba 12 mzazi wa mwanafunzi huyo alifika shuleni akiomba kuzungumza na watoto waliokuwa wakisoma darasa moja na mwanaye na aliruhusiwa.

Alisema baadaye mzazi huyo alisema mtoto wake alikimbizwa na mlinzi hadi mtoni.

Mkurugenzi huyo alisema anakumbuka Novemba 6 usiku alimuona mtu kama mwanafunzi na kumkimbiza, lakini hakumkamata.

Alisema mlinzi alitoa taarifa kwa uongozi wa shule na baada ya wanafunzi kuitwa kwa ukaguzi wote walikuwapo.

Mmiliki wa shule hiyo inayopokea wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali, Edward Shayo amelazwa Hospitali ya KCMC akisumbuliwa na shinikizo la damu.

Mwandishi wa SWAHIBA BLOG aliyefika KCMC jana mchana, alishuhudia ulinzi mkali katika wodi binafsi aliyolazwa.



Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)