DEREVA WA DARADARA ABOMOLEWA NYUMBA.ZAKE NNE KWA MALA MOJA DAR

Admin
By -
0


Jasho linamtiririka. Mikono yake na mdomo vinatetemeka, vishikizo viwili vya shati lake la mistari ya rangi ya zambarau na nyeupe vimeachia.

Sehemu kubwa ya tumbo lake ipo wazi, macho yake mekundu yanalengalenga machozi. Ghafla anaaza kulia huku akijiviringisha chini.

Licha ya kuwa na mwili mkubwa, anaonekana kuwa mwepesi kwa namna anavyoviringika chini. Kitendo hiki kinawavutia watu waliokaribu kusogea kuangalia kitu kinachoendelea.

Baada ya dakika kama mbili au tatu, akiwa amejaa vumbi mwilini anasimama na kuwafuata maofisa wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) waliokuwa wakibomoa nyumba mtaani kwake.

Anapiga magoti huku akizungumza na maofisa hao: “Msinibomolee nyumba zangu. Nitakwenda wapi na watoto wangu?” Ghafla anadondoka chini na kuzimia.

Huyu ni Nicomed Leo (61), mkazi wa Kimara Stop Over jijini Dar es Salaam na mwathirika wa bomoabomoa ya zaidi ya nyumba 1,000 zinazodaiwa kujengwa ndani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro mita 121.5 kila upande kuanzia Kimara hadi Kiluvya.

Siku hiyo ndiyo ambayo nyumba zake nne; mbili za ghorofa moja na mbili za kawaida alizodai zilikuwa na thamani ya Sh900 milioni zilikuwa kwenye ratiba ya kubomolewa, lakini kabla hazijafikiwa yakamkuta yaliyomkuta.

Baada ya kuzimia Leo alibebwa na kuwekwa sehemu ya wazi na kuanza kupepewa ili apate hewa ya kutosha. Baada ya muda mfupi anazinduka.

Baada ya kuzinduka akahoji: “Wamebomoa? Nyumba zangu jamani, nyumba zangu.”

Hata hivyo, msimamizi wa bomoabomoa hiyo, Janson Rutechula akawaamuru maofisa wenzake wasibomoe nyumba za Leo kisha akamfuata mmiliki huyo na kumweleza hawatabomoa nyumba zake kwa wakati huo.

Rutechula na wenzake waliondoka eneo hilo na kusitisha ubomoaji wa nyumba za Leo kwa muda.

“Tumeamua kuacha kwanza lakini haimaanishi hatutaboamoa. Tutazibomoa tu,” anasema Rutechula wakati akizungumza na Mwandishi wetu.

Siku ya pili baada ya tukio hilo, gazeti la Mwananchi likafunga safari tena kwenda nyumbani kwa Leo ili kumjulia hali na kumkuta mke wake Maria Nicomed.

“Sijui kama ataweza kuongea, hali yake bado haiko sawa maana baada ya tukio la jana amekesha baa anakunywa pombe mpaka muda huu ninaozungumza amelala,” anasema.

Hata hivyo, baada ya muda mfupi Leo alitoka nje huku akionekana amevimba macho, amevaa shati nyeupe ambalo halikufungwa vyema vishikizo na kusababisha tumbo lake kubaki wazi.

Akapita mbele ya mwandishi bila kuzungumza chochote na kutoka nje ya geti la nyumba yake. Akiwa nje akasimama karibu na nyumba za jirani zake ambazo zilibomolewa jana yake.

Ameweka mikono nyuma na kutembea huku na kule, mara akapita mtoto mdogo mbele yake akamuuliza swali.

“Mage leo haujaenda shule eeh! bomoabomoa imekuzuia?”

Mwandishi wetu anamsongelea kumsalimia akitaka kujua hali yake:

“Leo sitaki kabisa kuongea naomba uniache, hata nikiongea haisaidii zaidi nitachochea nyumba yangu ibomolewe,” anasema Leo.

Baada ya muda Leo anapokea taarifa ya zuio la Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi juu ya ubomoaji wa nyumba 278. Alisikika akijisemea mwenyewe, “zuio limetoka tuwaone sasa kama watabomoa.”

Baada ya wiki moja

Leo aliona kama muujiza, hakudondosha hata chozi wala kugalagala tena. Alikuwa na ujasiri wa aina yake ambao uliwashangaza hata waathirika wenzake.

Huku nyumba yake ikiwa imebandikwa karatasi za zuio la mahakama kutaka isibomolewe, Tanroads waliibomoa. Leo alihaha huku na kule kuokoa baadhi ya mali za nyumba yake kama vile nondo, mabati na mbao pamoja na milango.

“Kuanzia leo sina imani tena na Mahakama wala Serikali, nimekosa tumaini kabisa, nimekubali Serikali imeshinda,” anasema Leo huku akiokota tofali zilizoangushwa na tingatinga na kuzikusanya.

Kabla ya bomoabomoa

Baada ya kupata taarifa ya ubomoaji wa nyumba zaidi ya 1,000 zilizondani ya hifadhi ya barabara hiyo, mwandishi wetu alifunga safari hadi Kimara Stop over ili kujua kinachoendela. Akiwa eneo hilo aliona umati wa watu ukiwa umekusanyika karibu na nyumba ya Leo.

Katika umati huo Leo alionekana akiwa amesimama nje ya geti la nyumba yake. Pia, walionekana wafanyakazi wa Tanesco wakiwa na vifaa vyao vya kazi.

Katika kudodosa mwandishi wetu akapewa taarifa kuwa Tanesco wamefika hapo kung’oa mita zao na kukata umeme kwenye nyumba zinazotakiwa kubomolewa yaani zenye alama ya X.

Miongoni mwa nyumba iliyotakiwa kukatiwa umeme siku hiyo ilikuwa ni ya Leo. Hata hivyo, wakati wafanyakazi hao wakijiandaa kuanza kazi hiyo katika nyumba ya Leo, wananchi waliokuwa wamekusanyika walikubaliana kuwafukuza wafanyakazi wa Tanesco.

Makubaliano yao hayo yalizaa matunda kwani walifanikiwa kutimiza lengo lao, baada ya kuwafukuza mwandishi wetu alimtembelea Leo nyumbani kwake ili kujua amejipangaje kukabiliana na bomoabomoa hiyo.

Mwandishi alipofika nyumbani alimkuta Leo akiwa amehamisha baadhi ya vitu vyake vikiwamo nyaraka muhimu na kuvifungia ndani ya buti za magari yake mawili.

Leo alionyesha baadhi ya vitu alivyofungia kwenye magari kuwa ni pamoja na televisheni kubwa ya kisasa ya nchi 60, spika, nguo na baadhi ya vyombo.

“Nimeshajiandaa kisaikolojia, wakimaliza kubomoa nyumba zangu mimi nachukua mabati na tofali nasimamisha tena kibanda hapa hapa. Nitalala na kuishi na wanangu hadi umauti utakaponikuta,” anasema na kuongeza:

“Nimetandika magodoro chini ya sakafu ndiyo nalalia na nimeacha vyombo vichache vya kupikia, nawasubiri waje kubomoa.”

Nyumba za Leo zilikuwa na wapangaji saba wakiwamo wamiliki wa kituo cha tiba asilia cha  Samaritarian Nutracetical  Services  ambao walikuwa wakimlipa kodi ya nyumba  Sh10 milioni kwa mwaka.

Pia, alikuwa na wapangaji wengine ambao walimlipa Sh50,000 hadi Sh100,000 kwa mwezi fedha alizodai zilimtosheleza kuendesha maisha yake ikiwamo kusomesha watoto wake. “Nyumba yangu ilikuwa na wapangaji wote wameondoka na walipoondoka  watatu waling’oa milango ya nyumba na kuondoka nayo kwani  walikuwa wamelipia kodi ya miezi sita na walipotaka niwarudishie sikuweza hivyo wakangoa milango,” anasema.

Alivyojenga nyumba zake

Leo anaeleza kuwa mwaka 1988 alifika Dar es Salaam akitokea Mkoa wa Kilimanjaro, wakati huo alikuwa akijishughulisha na kazi ya ufundi wa magari.

Akiwa Dar es Salaam alibahatika kununua daladala kutokana na kazi yake hiyo. Baada ya kununua gari hiyo ya biashara aliachana na ufundi na  kuwa dereva wa gari yake.

Mwaka 1994 alipata fedha akanunua nyumba kwa mtu aliyemtaja kuwa ni Paulo Kihampa, baada ya kujiridhisha kwa kutumia kiogozi wa Serikali ya Mtaa Stop Over, Abuu Mbasi  kuwa haiko ndani ya hifadhi ya barabara.

“Nilinunua nyumba kwa bei ya Sh2 milioni. Baada ya hapo nikajenga nyumba ya ghorofa moja na baada ya miaka mitano  aliongeza nyingine ya gorofa moja.” anasema.

“Nilikaa miaka miwili nikaanza kujenga taratibu nyumba ya tatu ambayo haikuwa ya ghorofa, nilitumia miaka mitatu kukamilisha ujenzi huo nikiwa bado na kazi yangu ya udereva,” anasema.

Nilipokamilisha tu nikaanza tena kujenga nyumba ya nne ambayo pia niliijenga kidogokidogo mpaka sasa kiwanja chake kilikuwa na nyumba nne ndani ya eneo moja,” anasema.

Maisha mapya baada ya kubomolewa

“Najiuliza sijui kwanini bado naishi hapa, lakini sipati jibu. Nikilala nikiamka najikuta nipo hapa,” anasema Leo ambaye licha ya nyumba yake kubomolewa bado anaendelea kuishi katika mabaki ya nyumba yake.

“Nalala kwenye pagale hili, watoto wangu nimewapeleka kwa ndugu na jamaa, naamimi nimebaki hapa sina pakwenda napambana na hali yangu,” anasema.


Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)