Tanga. Hatimaye mtu anayehisiwa kuwa ndiye aliyepanga na kushiriki mauaji ya watu wawili kwenye chumba cha nyumba ya kulala wageni jijini hapa, amekamatwa katika mpaka wa Tunduma, katika kile kinachodhaniwa kuwa ni kujaribu kutoroka nchini.
Mtuhumiwa huyo, ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi, anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Tanga.
Kamanda wa polisi mkoani Tanga, Benedictor Wakyamba alisema jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja kutokana na tuhuma za mauaji ya watu hao wawili yaliyotokea ndani ya chumba namba 303 cha nyumba ya wageni ya Bomai iliyopo Kata ya Majengo jijini hapa Septemba 24 mwaka huu.
Wanaume wawili walikufa kifo cha kutatanisha katika nyumba ya kulala wageni baada ya miili yao kukutwa chumba kimoja ikiwa imefungwa kamba mikononi, tumboni na miguuni.
“Baada ya mauaji yale, Jeshi la Polisi hatukulala na tulihakikisha wahusika wanapatikana ndani ya muda tuliojiwekea na ushirikiano wetu na raia wema na vyombo vingine vya usalama tumefanikiwa kumkamata mtu huyu kabla hajatorokea nchi jirani,” alisema Wakyamba.
Alisema kukamatwa kwa mtu huyo wanayedhani kuwa ni kinara wa mauaji kutasaidia kupatikana kwa watuhumiwa wengine wa tukio hilo ambalo liliwashtua siyo wakazi wa Tanga pekee bali Tanzania nzima kutokana na aina ya uuaji ambao haujawahi kutokea.
“Tukio hili lilituchanganya sana Jeshi la Polisi kwa sababu hatukuwa tukijua mauaji hayo yalikuwa na sababu zipi na wauaji walikuwa na lengo gani. Lakini kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu kumetupa mwanga baada ya kumhoji,” alisema Wakulyamba.
Wakyamba alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa kujibu shitaka la kupanga na kushiriki mauaji hayo.
Tags
Kitaifa