Dar es Salaam. Vyuo vikuu 19 vilivyofungiwa kudahili wanafunzi mwaka huu, huenda vikapata unafuu wa rungu hilo mwakani endapo vitakidhi matakwa ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Akizungumza leo na Swahiba blog Kaimu Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Eleuther Mwageni amesema uhakiki wa kuzingatia sifa zinazohitajika kwa vyuo husika unaendelea kwa kuzingatia ukaguzi uliofanywa kati ya Juni na Julai kuona kama vimezingatia vigezo vilivyowekwa ili kuboresha elimu inayotolewa.
“Ukaguzi huu haufanywi ili kuondoa zuio lililowekwa bali kuboresha elimu. muda wa udahili ukifikia tamati, vyuo vilivyofungiwa vitatakiwa kufanya hivyo kuanzia mwaka ujao wa masomo baada ya kukidhi vigezo vinavyotakiwa,” amesema.
Taasisi zilizofungiwa kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa na TCU ni pamoja na Chuo Kikuu cha Eckenforde cha Tanga, Jomo Kenyatta, Kenyatta, Chuo Kikuu cha UMoja wa Mataifa (UN-WIDER), Chuo Kikuu IMTU na Chuo Kikuu cha Bagamoyo.
Vingine ni Chuo Kikuu cha Afya cha Mtakatifu Francis, Chuo Kikuu cha Askofu James, Chuo Kikuu cha Askofu Mihayo, Chuo Kikuu cha Kadinali Rugambwa, Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala (KIU), Chuo Kikuu Marian na Chuo Kikuu cha St John kituo cha Msalato na Chuo Kikuu cha St John Tanzania.
Kwenye orodha hiyo, Chuo Kikuu cha Marks, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha St Joseph, kampasi mbili za Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji; Mbeya na Tabora, Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Mbeya, na KCMC.
Ametumia nafasi hiyo kuvionya vyuo vilivyodahili wanafunzi wengi kuliko ukomo uliowekwa na tume hiyo akikumbusha kwamba kutovizingatia kutalazimu kuchukuliwa hatua za kisheria kwa taasisi husika.
Alipokuwa akizindua mabweni mapya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mapema Juni, Rais John Magufuli aliagiza kuachana na mfumo wa TCU kudahili wanafunzi na kuwapangia vyuo vya kwenda akisema unaleta urasimu na kuvipendelea hata vyuo visivyokuwa na sifa.
Amesema wanafunzi hao ni watu wazima wanaoweza kuchagua chuo cha kwenda hivyo taasisi hizo ziachwe huru kujitangaza na kuvutia wanafunzi wa kutosha kukidhi mahitaji yao.
Utekelezaji wa agizo hilo umeanza kutekelezwa mwaka huu wa masomo lakini taarifa zilizopo zinasema vipo baadhi ya vyuo vimezidisha idadi ya wanafunzi vinavyostahili kuwa nao.
“Ni kosa kuzidisha wanafunzi. Hakuna chuo kinachoruhusiwa kuzidisha wanafunzi kwenye kozi yoyote. Tutafanya ukaguzi wa kushtukiza kujiridhisha na hilo,” amesema Profesa Mwageni.
Onyo la TCU pia lilielekezwa taasisi nyingine 22 kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambavyo vilizuiwa kudahili wanafunzi kwenye baadhi ya kozi zinazofundishwa kwa mwaka huu wa masomo 2017/18
Tags
Kitaifa