Matajiri wa manchester klabu ya Manchester City jana usiku walijiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwenda hatua ya robo fainali katika michuano ya ulaya baada ya kupata ushindi wa ugenini wa goli 3-1 dhidi ya klabu ya Dynamo kyiv.
City waliandika bao la kwanza dakika ya 15 tu ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wao Sergio Aguero.
Dakika ya 40 ya mchezo huo mchezaji machachari wa City David Silva aliongeza bao la pili na hivyo ufanya mechi hiyo hadi mapumziko kusomeka 2-0.
Dynamo kyiv walirudi kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata goli mnamo dakika ya 59 kupitia kwa mchezaji wao Buyalsky.
Mchezaji bora mara tatu wa Afrika Yaya Toure alipigilia msumari wa mwisho katika dakika ya 90 na kuifanya Manchester City kuchomoza na ushindi wa 3-1 wakiwa ugenini na hivyo kujiwekea mazingira mazuri ya kuitoa Dynamo Kyiv katika mchezo wa marudiano.
Katika mechi nyingine Atletico Madrid walitoka sare ya bila kufungana dhidi ya PSV Eindhoven.