Mabingwa wa zamani wa kandanda Tanzania bara, Coastal Union ya Tanga imeondoka Tanga Alhamis kuelekea mkoani Shinyanga kucheza na timu ya Mwadui FC ambayo imepoteza michezo miwili kati ya mitatu iliyopita ya ligi kuu Tanzania bara.
‘Wagosi wa Kaya’ waliifunga Yanga SC kwa magoli 2-0 katika mchezo wao wa kwanza wa mzunguko wa pili, kisha badae wakawachapa 1-0 Azam FC wiki iliyopita wanaamini wanaweza pia kuwafunga vijana wa kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ katika uwanja wao wa Mwadui Complex siku ya Jumamosi.
“Maandalizi yetu yanakwenda vizuri. Tunajiandaa kwa safari ya kuelekea Shinyanga. Tunataraji kuondoka Tanga siku ya Alhamis. Tuna morali zaidi baada ya kuwafunga Azam”, anasema meneja wa Coastal Union, Rawash Mohamed ambaye pia anasema ‘upepo mbaya’ umeshapita katika timu yao.
“Mashabiki wetu nawaomba waendelee kutuunga mkono, nawahakikishia upepo mbaya tayari umeshapita katika timu yetu hivyo tumejiandaa kwa mchezo ujao dhidi ya Mwadui FC naimani tutafanya vizuri.”
Tags
Michezo
