Siku za kocha Dylan Kerr meanza kuhesabika ndani ya Simba Kerr akalia kuti kavu Simba Kutokana na mwenendo wa kusuasua wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.
Vuguvugu la kumuondoa Kerr limekuja siku chache baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Prisons Jumatano, jambo ambalo limesababisha Simba iporomoke hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 15.
Licha ya Kerr kuiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi katika mechi tano na mechi tatu akivunja rekodi mbaya kwenye viwanja vya Mkwakwani, Tanga na Sokoine, Mbeya, ambavyo kwa miaka miwili ilikuwa haijawahi kupata matokeo ya ushindi, kazi hiyo kubwa iliyofanywa na Kerr inaonekana kutowashawishi viongozi wa Simba ambao wanadaiwa kuwa wanajiandaa kuachana na raia huyo wa Uingereza.
Mmoja kati ya viongozi wa Simba alilithibitishia gazeti hili nia ya timu hiyo kutaka kuachana na Kerr, lakini akasema kuwa suala hilo bado liko kwenye majadiliano na si la kukurupuka.
“Kuna mambo mengi tumekuwa hatupendezwi nayo kutoka kwa huyu mwalimu. Kama timu hatuwezi kuacha tatizo lizidi kukua na ndio maana tunajipanga kuachana naye,” alisema mtoa habari huyo.
“Kwanza alipewa mechi mbili ya Mbeya City na Prisons ndipo atimuliwe, lakini viongozi wameona kuwa ngoja amalizie kama mechi mbili zilizobaki kabla ya kambi ya Stars na ligi ikisimama kwa ajili ya kambi hiyo aondoke.
“Jambo linalomuondoa ndani ya timu hiyo, kwanza anawapa wachezaji mazoezi mepesi ambayo hayana faida na timu inaonekana inacheza kwa dakika kadhaa halafu wachezaji wanachoka, sasa kwa hali hiyo tunaweza kupoteza michezo mingi kwenye ligi,” alisema kiongozi huyo.
Aliongeza: “Pia si mkali kwa wachezaji, amejenga urafiki na wachezaji na hata wakifanya makosa anashindwa kuwasema, sasa kama nidhamu kwa wachezaji hamna, basi hakuna timu hapo. Kocha lazima awe mkali pale inapobidi ili wachezaji wamuheshimu na waheshimu kazi yao.”
Pia, kiongozi huyo alisema Kerr alishawaambia viongozi wa Simba kuwa kuna ofa ya maana amepata nchini Vietnam hivyo jambo hilo nalo limeifanya kazi ya kumtimua kuwa rahisi.
Kocha Kerr alikiri kusikia taarifa kuwa uongozi wa timu hiyo upo kwenye mipango ya kuachana naye na anachosubiri kwa sasa ni uongozi wa klabu hiyo kutoa uamuzi kama anabaki au anaondoka.
“Nasubiri nione wanaamua nini, kama nitabaki katika mechi mbili zijazo ni lazima nihakikishe tunapata ushindi, kufanya vibaya katika mechi iliyopita kunatakiwa kutujenga zaidi siyo kutubomoa,” alisema Kerr.
Hata hivyo, Rais wa Simba, Evance Aveva alisema hawana mpango wa kumtimua kocha huyo kwa sasa na nguvu zao wameelekeza kufanya vizuri kwenye ligi. “Hatuna mpango huo kwa sasa, hayo ni maneno tu yanasemwa, sasa hivi tunaangalia kufanya vizuri kwenye ligi,” alisema Aveva.
Minziro, Mwaisabula wamtetea Kerr
Kocha wa zamani wa JKT Ruvu, Fred Felix Minziro alisema vigezo vilivyotumika kuwaacha washambuliji, Elius Maguli na Amiss Tambwe msimu huu na kisha kuwasajili, Musa Hassan Mgosi na Pape N’daw akiufananisha usajili huo na msemo wa kuruka majivu na kukanyaga moto.
“Sijui ni vigezo gani vilitumika kuwasajili N’daw na Mgosi na kuwaacha Maguli na Tambwe hilo wanalijua Simba wenyewe, lakini hawakuwa wachezaji wa kuachwa,” alisema Minziro.
Mchambuzi, Ken Mwaisabula alisema kinachoiumbua Simba sasa ni kufanya usajili wa maslahi ya baadhi ya viongozi bila kuangalia aina na kiwango cha mchezaji.
“Tatizo la klabu zetu hasa hizi kubwa kipindi cha usajili baadhi ya watu wanaangalia maslahi yao, kitendo cha kumwacha Tambwe au Maguli na kwenda kuwasajili kina N’daw kinashangaza.
“Suala la Tambwe walimsingizia Patrick Phiri, lakini haikuwa kweli, hili la Maguli kocha (Kerr) alisema anakosa nafasi nyingi za wazi, kwani kazi ya kocha si kumtengeneza mchezaji arudi katika kiwango kizuri kama alikuwa akikosa magoli?, alishindwa nini kufanya kwa Maguli na kupendekeza aachwe na kwenda kumsajili N’daw ambaye hana msaada katika timu?,” Alihoji Mwaisabula.