Wakati Ligi Kuu Bara ikifika raundi ya nane safu ya ushambuliaji wa Yanga imeweka rekodi ya kufunga mabao 18 ikiwa ni wastani wa mabao matatu kwa mechi moja.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoongozwa na Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Malimi Busungu na Simon Msuva imeonekana tishio msimu huu kwani hadi sasa imefunga mabao 18 ikiizidi Azam mabao saba na ikiwazidi wapinzani wao, Simba mabao 10.
Ubora wa Yanga si tu katika kufumania nyavu, hata safu ya ulinzi ya timu hiyo imeonyesha uimara zaidi baada ya kuruhusu mabao matatu katika michezo saba iliyocheza.
Azam inafuatia kwa kuwa na safu mahiri ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao 11, wakati Stand United imefunga 10 huku Simba na Mwadui zikiwa zimefunga mabao manane kila moja.
Hata hivyo, Azam nayo imeonekana kuwa na ukuta imara unaojengwa na Muivory Coast Serge Pascal Wawa, Aggrey Morris, Said Morad, David Mwantika, Shomari Kapombe na Aishi Manula ambao umeruhsu mabao matatu tu sawa na Yanga.
Ukuta wa Yanga unaongozwa na Ali Mustapha ‘Barthez’, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mwinyi Haji, Juma Abdul na Mbuyu Twite umeonekana ni mchungu kwa washambuliaji wengi wakorofi.
Katika ligi hiyo, JKT Ruvu haijashinda mchezo wowote kwenye mechi nane ilizocheza. Timu hiyo imeonekana dhaifu kwa kuruhusu timu nyingi kujipigia tu kwani imefungwa mabao 12 ikifuatiwa na Kagera Sugar iliyoruhusu mabao 10.
Timu hiyo ilimtimua kocha Fred Felix Minziro kutokana na mwenendo mbovu kwenye ligi na sasa ipo chini ya kocha mkongwe, Abdallah ‘King’ Kibadeni.
“Nimechukua kazi ngumu kuinoa JKT Ruvu na sababu haipo vizuri kwenye ligi, lakini naamini kama wachezaji watafuata malekezo na kujituma, tutatoka sehemu tulipo na kumshangaza kila mmoja,” alisema kocha wa timu hiyo, Kibadeni.
Pia, msimu huu African Sports na Coastal Union ndio timu zenye mabao machache kuliko zote kwani katika michezo minne kila moja imefunga bao moja tu.