Huyu ndio kocha mpya aliyeletwa nchini na Boss wa wekundu wa Msimbazi bilionea Mohamedi Dewji akitokea nchini Ufaransa.
Hubert Velud alizaliwa tarehe 8 Juni, 1959 katika mji wa Villefranche-sur-Saône mashariki mwa nchi ya Ufaransa.
Historia yake kisoka kocha huyu mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika, alianza kucheza soka kama mlinzi wa kati katikati ya miaka ya 70 kabla yakuamua kuwa golikipa akiwa na klabu ya Stade Reims ambayo alidumu nayo mpaka mwaka 1989.
Mwaka 1989 aliingia mkataba na klabu ya Charlons sur Marne ambayo alidumu nayo kwa miezi 11 tu kabla yakuamua kustaafu soka na kujikita katika masuala ya ukocha.
Ana leseni daraja A ya ukocha inayotambuliwa na Shirikisho la soka barani Ulaya ( UEFA ) .
UZOEFU AFRIKA
Hubert Velud ni mzoefu na soka la Afrika akikumbukwa jinsi alivyoweza kukiweka sawa kikosi cha timu ya taifa ya Togo mwaka 2009-10 alipokuwa akikinoa.
2011 Velud aliingia mkataba na klabu ya ligi kuu nchini Morocco klabu ya Hassania Agadir ambayo aliiwezesha kuwa ndani ya nne bora ya msimamo wa ligi. Mwaka 2012 mwanzoni matajiri wa ES Setiif toka nchini Algeria walimnyakua kocha huyu kuja kuinoa klabu hiyo. Akitumia mfumo wake maarufu wa 4-3-3 aliweza kuwapa ubingwa wa ligi kuu ( League one ) msimu wa 2012-13.
Akiwa amewakatia tiketi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika wapinzani wao USM Alger walimnyakua mfaransa huyu ili kuimarisha ushindani kitu ambacho kiliwaudhi Setiif na waliyumba kiufundi. Velud aliweza kuwapa kombe la Algerian Super Cup katika kipindi kifupi tu hali iliyozidisha ubora wa soka lake Afrika.
2015 aliachana na USM Alger baada ya kupata ofa nono ya wakali wengine wa ligi ya Algeria CS Constantine moja ya timu kongwe sana nchini humo ikiundwa mwishoni mwa karne ya 19. Hawa alikaa nao kwa miezi 8 akianza kukisuka upya kikosi hicho ambacho msimu wa 2014-15 kiliondokewa na nyota wake wengi. Akiwa katikati ya msimu bilionea Moise Tchitumbi wa TP Mazembe alimwekea ofa kubwa mezani ili akiongoze kikosi chake katika michuano ya klabu bingwa Afrika na ligi za ndani baada ya kusikia ubora wake .
Alijiunga na TP Mazembe mwaka 2016 na kuwapa ubingwa wa Linafoot na Super Coupe du Congo. Yalikuwa mafanikio ya haraka na wakali hao wa Lubumbashi lakini hakuweza kudumu nao baada ya timu za Afrika kaskazini kutupa tena ndoano yao kumnasa kocha huyo aghali!.
Etoille du Sahel wanaoshiriki ligi kuu nchini Tunisia walimnasa kocha huyu kwa msimu wa 2016-17 ingawa hakuwa na mafanikio makubwa sana na klabu hiyo hali iliyomfanya mwishoni mwa msimu kutimkia kwao nchini Ufaransa.
Huyu ndio Hubert Velud ambaye Simba wamemleta nchini kukinoa kikosi chao katika harakati za kuusaka ubingwa wa ligi Tanzania na ushiriki wao katika michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika.
Ni kocha ambaye anahusudu soka la vijana, kasi , nguvu , pasi fupi fupi zenye kasi katika kushambulia akiwa muumini mkubwa Total football. Mkali sana katika masuala ya nidhamu na yupo radhi kuvunja mkataba wake pale anapoingiliwa majukumu yake akihofia kuharibiwa CV yake.
0 Comments