MAKONDA AJITAPA KUTIBUA MBINU ZA WANAOFUKUZIA URAISI CCM

Admin
By -
0


 Wakati Uchaguzi Mkuu ukitarajiwa kufanyika mwaka 2025, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amedai kuwa, ziara yake ya siku nane katika mikoa ya kanda ya ziwa imewavuruga baadhi ya watu wanaosaka urais ndani ya chama hicho tawala.


Makonda aliyeteuliwa Oktoba 22 kushika nafasi hiyo alianza ziara hiyo Novemba 9, 2023 katika Mkoa wa Kagera kisha kwenda Geita, Mwanza, Simiyu na Mara alikomaliza. Lengo la ziara hiyo ni kutoa shukrani sambamba na kuzungumza na wanaCCM na wananchi wa mikoa hiyo.


Katibu huyo ametoa kauli hiyo leo Jumatano Novemba 15, 2023 muda mfupi baada ya kuweka shada la maua katika kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipotembelea Kijiji cha Mwitongo wilayani Butiama na kuzungumza na familia ya marehemu.


Makonda amedai kuwa ziara yake imewavuruga watu wenye ndoto ya urais, akisema walifikiri watamchezea mwenyekiti wa CCM mwaka 2025 ili kukiyumbisha chama hicho ili kupata nafasi.


"Nawaambia la hasha! Na mmenipa hii fimbo nitawachapa kweli kweli," amedai Makonda na kuibua kicheko kwa wanafamilia ya Nyerere wakiongozwa na Madaraka Nyerere aliyempa fimbo Makonda kama ishara ya upendo.


"Ombi langu kwenu wazee msiache kuniombea mafisadi katika hii nchi bado hawajaisha, watu wanaopenda kudhulumu bado hawajaisha. Pia, wale wasiokuwa na sifa ya uongozi na wanataka uongozi hawajaisha,” amesema Makonda aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.


"Wakituona watu tunaosimamia haki hawapendi, watatafuta kila namna ya kuchonganisha viongozi kwa viongozi, mpasuko huu kwao ni mafanikio.Nina furaha tunaye Rais (Samia Suluhu Hassan) shupavu, mahiri na mtulivu anayepima mambo kwa upana wake.”


Makonda amesema atahakikisha CCM inakuwa chama cha kutetea wanyonge, sauti ya wananchi, kisichobagua na kitakachosimamia haki.


Amesema atahakikisha heshima ya Nyerere na kazi nzuri alizozifanya zinaendelea kuwa kumbukumbu.


Makonda amesema alama njema, uadilifu na sifa za Nyerere na utumishi wake bado unasomeka kwenye kurasa za Taifa hili hata nje ya mipaka nchi, ndiyo maana amekwenda kumuenzi.


"Wapo viongozi wanaomuenzi Nyerere katika majukwaa, lakini matendo yao hayafanani na mwalimu, mimi sitaki kuwa kama wao nataka kuwa tofauti kwa sababu hofu ya Mungu ndiyo msingi wa maisha yangu," amesema Makonda.


Msemaji wa familia ya Nyerere, Chifu Japhet Wanzagi amemshukuru Makonda kutenga muda wake wa kutembelea na kulala katika makazi ya Baba wa Taifa.


Amemshukuru pia kuweka shada la maua katika kaburi la Nyerere ikiwa ni ishara ya kuonyesha kutambua mchango wa mwasisi huyo wa Taifa.


"Tunakushukuru kwa ujio wako, umefanya moja kubwa pia la kulala katika makazi haya, hii ni baraka pia. Kwa niaba familia tunamshukuru Rais Samia kwa sababu hajakuacha, pia viongozi wa Serikali wamekuwa bega kwa bega nasi," amesema Wanzagi ambaye pia ni Chifu wa ukoo wa Nyerere Burito.

Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)