Miili ya watu 17 imepatikana baada ya boti kuzama katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, kulingana na maafisa wa eneo hilo.
Idadi kamili ya watu waliokuwemo kwenye boti hiyo bado haijabainika, lakini watu wawili waliokolewa wakiwa hai huku miili 17 ikipatikana.
Miili hiyo ilipatikana na jeshi la wanamaji mapema Jumatatu asubuhi na inaaminika kuwa wahamiaji kwa sababu ya aina ya mashua waliyokuwa ndani, alieleza Meya wa kitongoji cha Ouakam, Ndeye Top Gueye.
Kikosi cha wazima moto na wapiga mbizi kilikuwa kikiendelea kutafuta miili katika eneo hilo Jumanne mchana.
Wakati hii ikiwa ni mara ya kwanza miili kusombwa na maji katika kitongoji hicho, vifo vya wahamiaji baharini vinazidi kuwa vya kawaida nchini Senegal.
Haikuwa wazi watu hao walikuwa wanatoka wapi, walikuwa wa mataifa gani, au hata walikokuwa wakienda.
Lakini njia ya uhamiaji ya Atlantiki ni mojawapo ya njia mbaya zaidi duniani, na karibu watu 800 wanakufa au kutoweka katika nusu ya kwanza ya 2023 kulingana na shirika la misaada la Uhispania la Walking Borders.
Operesheni za utafutaji pia zimefanyika hivi karibuni nchini Uhispania, kutafuta boti za wahamiaji kutoka Senegal ambazo zimepotea, zikiwa na zaidi ya watu 300, kulingana na NGO ya Caminando Fronteras.