Askari ambaye aliwaua watu 13 nchini DRC alikamatwa jana mwendo wa saa nane mchana Msemaji wa Jeshi la Kongo alisema.
Luteni Jules Ngongo aliambia BBC kwamba mwanajeshi huyo anazuiliwa Kasenyi, kituo cha jeshi la wanamaji, katika Mkoa wa Ituri wenye matatizo. Askari huyo ambaye jina lake halikufahamika aliua watu 13 wakiwemo watoto 9 Jumamosi iliyopita katika kijiji cha Nyakova.
Wakazi wanasema mwanajeshi huyo alifyatua risasi wakati wa mazishi kwa sababu alikasirika kupata kuwa mwanawe alizikwa kabla ya kufika kijijini, kutoka uwanja wake wa vita.
Ni nini kilimchochea?
Majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini yamekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu 2021
Gazeti la Bunia-Actualité linaripoti kwamba askari huyo aliondoka eneo alilokuwa akifanya kazi na kwenda nyumbani baada ya kupata habari kwamba mwanae amefariki.
Inasemekana mwanae alifariki Alhamisi tarehe 20 na akazikwa Ijumaa jioni, bila baba yake kufika.
Mwanawe alidaiwa kufariki dunia kwa kifo cha kawaida baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Tchomia ambako alifariki dunia.
Baba aliporudi nyumbani na kumkuta mtoto wake amezikwa, alikasirika na kupiga risasi kati ya majirani waliofika kuifariji familia.
Radio Okapi inaripoti kuwa miongoni mwa wengine waliopigwa risasi na mwanajeshi huyo ni watoto wake wawili.
Luteni Ngongo anasema hilo ni suala la ‘kinidhamu’. Anasema askari huyu akikamatwa atashitakiwa mahakamani.