Idadi ya watu waliofariki kutokana na maambukizi ya virusi vipya vya Corona imeongezeka na kufikia 97 , ikiwa ndio idadi kubwa ilioripotiwa kwa siku nchini China.
Kufikia sasa idadi kamili ya vifo nchini humo ni 908 lakini viwango vya maambukizi mapya vimepungua.
Nchini China takriban watu 40,171 wameambukizwa huku 187,518 wakiwekwa katika uchunguzi wa kimatibabu. Shirika la afya duniani WHO limetuma kundi la wataalam mjini Beijing kusaidia kuchunguza virusi hivyo vipya.
- Daktari aliyetoa tahadhari ya mlipuko wa virusi kwa mara ya kwanza apoteza maisha
- China yailaumu Marekani kwa kueneza 'taharuki' kuhusu virusi vya corona
- Afisa wa Trump: Coronavirus itabuni ajira Marekani
Kulingana na data ya China wagonjwa takriban 3,281 wametibiwa hospitalini na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Number of coronavirus cases per day
Siku ya Jumatatu , mamilioni ya watu walirudi kazini baada ya kusherehekea mwaka mpya , ambao uliongezwa muda ili kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo.
Lakini hatua za tahadhari zinaendelea, ikiwemo kupunguza muda wa kufanya kazi mbali na kuchagua maeneo ambayo kampuni zinafaa kuendelea na kazi.
Wikendi iliopita , idadi ya visa vya vifo vilivyosababishwa na virusi hivyo iliipiku ile ya virusi vya SARS mwaka 2003 ambavyo pia vilianza nchini China na kuwaua watu 774 kote duniani.
Shirika la afya duniani siku ya Jumamosi lilisema kwamba idadi ya visa vipya ilikuwa inapungua , lakini likaonya kwamba ni mapema sana kusema hivyo wakati ambapo maambukizi ya virusi hivyo yako juu.
Virusi hivyo pia vimesambaa hadi mataifa 27 , lakini kufikia sasa kumekuwa na vifo viwili pekee nje ya China , katika taifa la Ufilipino na Hong Kong.
Mlipuko huo ulitangazwa kuwa jangwa na shirika la afya duniani tarehe 30 Januari. Virusi hivyo vipya mara ya kwanza viliripotiwa mjini Wuhan , mji mkuu wa mkoa wa Hubei.
Mji huo wenye takriban watu milioni 11 umetengwa kwa wiki kadhaa sasa.
Wakati huo huo mjini Hong Kong abiria waliotengwa katika meli moja wameruhusiwa kutoka baada ya vipimo kuonyesha kwamba hawana maambukizi pamoja na wafanyakazi wa meli.
Meli hiyo ya watalii kwa jina World Dream ilikuwa imtengwa baada ya abiria wanane kutoka meli nyengine ya watalii kuambukizwa .
Meli nyengine ya watalii iliopo pwani ya Japan imetengwa baada ya makumi ya visa kuthibitishwa.