Tofauti 4 Kati ya mfanya biashara na mjasiriamali

Admin
By -
0
Wengi wapo kwenye biashara hata hivyo hujiita wajasiriamali. Hii ni kwa sababu kumekua na mchanganyiko mkubwa kuhusu nani haswa ni mjasiriamali na nani mfanyabiashara.
Makala hii itakufanya usichanganye maneno hayo mawili, na ufahamu kama wewe ni mfanyabiashara au mjasiriamali na mwisho ni matumaini yetu Makala hii itakufanya uwe na hamu ya kuwa mjasiriamali badala ya kuwa mfanyabiashara.
Tutaanza kwanza kuangalia ufanano wa mjasiriamali na mfanyabiashara.
Mambo ambayo   mjasiriamali na mfanyabiashara wanafanana
  • Wote wawili hujikita katika kufikisha bidhaa au huduma fulani kwa walengwa wao. 
  • Wote wawili hufikiria manufaa wanayoweza kupata kutokana na hicho wanachokifanya.
  • Wote wawili wanaweza kunufaika kutokana na hicho wanachokifanya.
  • Mwisho wa siku wajasiriamali wengi na wafanyabiashara wote hujihusisha na biashara -yaani kuuza kitu fulani kwa faida.

Mambo ambayo mjasiriamali na mfanyabiashara wanatofautiana

Utofauti wa lengo kuu kati ya mjasiriamali na mfanyabiashara
Mjasiriamali ingawa anaweza kunufaika yeye kama yeye kutoka na anachofanya, lengo lake la msingi huwa sio yeye kama yeye afanikiwe, bali lengo lake ni kuona suluhu Fulani ya tatizo ambalo anataka kulitatua. Hivyo basi mjasiriamali hujikita Zaidi katika jamii, kuangalia nini anaweza kufanya cha kuleta ahueni. Mjasiriamali huhamasika zaidi na vile ambavyo anaweza kutatua changamoto fulani. Kwa upande wa mfanyabiashara lengo kuu ni kupata faida, hakuna mtazamo wa kina kuhusu changamoto gani au kwa namna gani jamii husika itapata haueni.  Ingawa anachofanya mfanyabiashara kinaweza kuleta ahueni na kutibu changamoto Fulani, lakini hilo sio wazo lake kuu au sio ambacho haswa kimemuingiza katika biashara. Yeye mfanyabiashara kinachompa hamasa kweli ni “kupiga hela” fasta.
Utofauti katika ubunifu kati ya mjasiriamali na mfanyabiashara
Mjasiriamali hujihusisha zaidi na kubuni bidhaa au huduma mpya au namna mpya ya kuwasilisha bidhaa na huduma zilizopo, au kufikia kwa namna ya kipekee soko jipya kwa bidhaa ambazo tayari zipo. Unaona katika kila jambo mjasiriamali hujihusisha na UPYA Fulani.  Kwa upande wa mfanyabiashara hujishughulisha na vitu ambavyo tayari vimekwisha buniwa bila kuongeza kitu cha ziada. Hii ni kwa sababu lengo la mfanyabiashara ni kufanya chochote kile kitakachomuingizia faida. Mfano kwakua kaona mwingine anauza nguo na zinatoka, basi yeye ataenda kununua nguo za aina ile auze tena kwa soko lile lile ambalo mwenzake anauza.
Mahusiano na watu wa karibu katika shughuli
Mjasiriamali kwakua ana lengo la kutengeneza kitu fulani na mtazamo wake upo katika jamii, mara nyingi hujikita katika kutafuta timu bora ya kufanya nayo kazi kwakua mjasiriamali ana mtazamo mpana wa kuona kitu alichonacho kinafikia mbali na anajua bila watu wazuri wakaribu yake hatoweza. Wakati huo mfanyabiashara kwakua hujikita zaidi katika kutafuta faida, na yeye mara nyingi manufaa yake binafsi ndio jambo la msingi zaidi, huwa hatilii maanani sana mambo ya mahusiano na kukua kwa pamoja na wale anaofanya nao shughuli yake. 
Mjasiriamali huboresha na kuzingatia hata mahusiano yake na mteja, na kwamba mteja na mfanyakazi ni sehemu muhimu ya biashara wakati kwa mfanyabiashara mteja ni mtu tuu wa pembeni wa nje ya biashara yake, na wafanyakazi kama tuu watoa huduma wa kumnufaisha yeye mfanyabiashara afikie malengo.
Hatari ya kupata hasara ilivyo kati ya mjasiriamali na mfanyabiashara
Kwakua mara nyingi mjasiriamali ni mwanzishaji wa bidhaa au huduma mpya au namna mpya ya kufikisha bidhaa au huduma iliyopo katika soko jipya au ambalo tayari lipo, mara nyingi mjasiriamali huwa hatari kubwa sana ya kupata hasara ukizingatia huo upya wa kufanya jambo.
Kwa upande wake mfanyabiashara ingawaje nae anaweza kupata hasara katika shughuli yake , hatari yake ya kupata hasira haiwezi linganishwa na mjasiriamali kwakua yeye mfanyabiashara anahusika na bidhaa au huduma ambayo tayari imekwishafahamika utaratibu wake wa jinsi ya kutengeneza na kuuza.  
Tags:

Post a Comment

0Comments

Post a Comment (0)